Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini
Mashariki, Lucy Nkya amesema kuwa milio ya risasi iliyosikika ofisini
kwake, ilitokana na mtoto wake Jonas Nkya, kuangusha bastola kwa bahati
mbaya.
Nkya alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kusikika kwa milio ya risasi ofisini kwake
huku kukiwepo kwa taarifa kwamba alivamiwa na mtoto wake huyo akidaiwa
kutaka kumuua kwa kumpiga risasi.
mbunge NKYA |
Mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, alisema kuwa hawana ugomvi wowote na mtoto wake na
iwapo wangekuwa na ugomvi angewatumia wazee na wakubwa wa familia
kusuluhisha.
“Jonas amehamia nyumbani kwangu kwa ajili ya
kunisaidia kumlea baba yake ambaye ana tatizo la kupooza. Kama tungekuwa
na ugomvi, tungegombana nyumbani na siyo ofisini,” alisema Lucy.
Alitoa ufafanuzi kuwa Jonas alifika ofisini kwake
kwa lengo la kuchukua gari kubwa ili aende shamba, lakini wakati akitoka
ofisini humo, aliinama na ghafla bastola aliyoiweka kiunoni ilidondoka
na risasi kuanza kufyatuka.
Dk Nkya pia alikanusha taarifa zilizodai kuwa
katika ugomvi huo alikuwa akirushiana risasi na Jonas akisema kuwa,
binafsi alishika silaha mara ya mwisho mwaka 1972 alipokuwa katika Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT), Mafinga aliposhiriki zoezi la shabaha.
Alisema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa
kwenye familia yake na kwa viongozi wenzake wakiwemo wabunge pia
kumfanya ashindwe kufanya kazi zake. Kwa upande wake Jonas Nkya, ambaye
ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, alikiri kufika ofisini kwa mama yake
akiwa na bastola akieleza kuwa alikwenda kuchukua gari ili aende shamba
na kwamba hakuwa na dhamira ya kufanya shambulizi lolote kwa mama yake
kwani hawakuwa na ugomvi.
Alisema kuwa risasi zilifyatua baada ya kuanguka
kwa bastola hiyo aliyokuwa ameiweka kiunoni na baada ya tukio hilo
alikwenda katika Hospitali ya St Mary kwa ajili kupatiwa matibabu
kutokana na mshtuko alioupata baada ya risasi kufyatuka.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Leonard Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema
kuwa uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua kama risasi hizo zilifyatuka
kwa bahati mbaya ama kwa nia ovu. “Pamoja na uchunguzi, tunamtafuta
Jonas kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu tukio hilo,” alisema .
0 comments:
Post a Comment