WANAWAKE wengi wamekuwa wakilalamikia maumivu ya kiuno hawa wanapokuwa katika kipindi chao cha hedhi kisha kufifia. Kuna maumivu ya kiuno ambayo hukaa kwa muda mrefu yaani miezi sita na kuendelea au kuwa yanajirudia mara kwa mara.
Maumivu haya huweza kusababishwa na mambo mengi kama vile kuwa na matatizo kwenye via vya uzazi, kibofu cha mkojo, utumbo mkubwa au misuli ya nyonga. Yanaweza kuwa yanaendana na mzunguko wa hedhi au la, wengi huwatokea chini ya kitovu na kiunoni na yanaweza kuwa makali.
Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mwanamke kupata maumivu ya kiuno kwa muda mrefu, baadhi ya sababu hizo ni kuwa na maumbukizi ya ndani ya kiuno ya muda mrefu (Chronic Pelvic Infection) yanaweza kuwa ni kwa sababu ya kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu ( TB) au kuwa na Endometriosis. Hii ni hali ambayo seli za ukuta wa uzazi huota sehemu nyingine za uzazi. Huleta maumivu wakati wa hedhi au wakati wa kufanya mapenzi.
Mwanamke pia anaweza kuwa na maambukizi ya muda mrefu ya shingo ya uzazi au mji wa uzazi (Chronic Endometritis or Cervicitis). Hali hiyo husababisha maumivu ya kiuno wakati wowote na wakati wa kufanya mapenzi au yanaweza kutokea ikiwa mimba imetungwa nje ya Mfuko wa Uzazi (Ectopic Pregnancy).
Lakini pia vivimbe vya kizazi (Uterine Fibroids) vinaweza kusababisha maumivu pale ambapo vinakua kwa haraka, vinajiviringisha au kukandamiza ogani nyingine. Maambukizi ya njia ya mkojo ya muda mrefu (Chronic Urinary Tract Infection) huweza kusababisha maumivu hasa wakati wa kukojoa,(Tatizo hili la kuumwa njia ya mkojo tutafafanua katika matoleo yetu yajayo).
Mwanamke pia anaweza kuwa na maumivu kutokana na kuwa na maambikizi ya via vya uzazi kitaalamu huitwa Pelvic Inflammatory Disease – PID. Pia maambukizi ya kibofu cha mkojo (Interstitial Cystitis) huleta maumivu hasa chini ya kibofu cha mkojo ambayo hupungua pale unapokojoa.
Dalili nyingine ni kukojoa mara kwa mara, kukojoa usiku na kushindwa kubana mkojo. Mtu mwenye ugonjwa wa Kidole Tumbo (Chronic Appendicitis) anaweza kukumbwa na tatizo hilo na hupata maumivu upande wa kulia chini ya kitovu.
Wengine hupata maumivu kutokana na kushikana kwa via vya uzazi (Pelvic Adhesions) au kuwa na saratani ya utumbo mpana na mgonjwa kujisikia maumivu ya tumbo hasa chini ya kitovu na kiunoni kwa muda mrefu.
Maumivu hutokea kama mwanamke ana tatizo la kusagika kwa mifupa kwenye maungio (Degenerative Joint Disease) na kusababisha maumivu makali maeneo ya kiunoni hasa wakati wa kutembea.
TIBA YAKE
Maumivu ya kiuno ya muda mrefu hutibiwa kwa kugundua chanzo cha maumivu kwanza au kwa kujua historia ya tatizo, uchunguzi pamoja na vipimo hufanyika. Matibabu hutegemea na chanzo cha tatizo; Dawa za kutuliza maumivu, dawa za majira kama tatizo linahusiana na mzunguko wa hedhi au upasuaji.
0 comments:
Post a Comment