MSANII MAARUFU NCHINI, DIAMOND |
Na Saleh Ally
GAZETI
la Championi lilianza kujulikana kabla ya ujio wa Nasibu Abdul
‘Diamond’. Ninaamini litaendelea kubaki nikiwa ninamaanisha hivi,
ataliacha likiendelea kusikika kwa miaka mingine mingi.
Championi
litaendelea kusikika kwa kuwa linaundwa na watu wengi makini wanaotaka
liendelee kufanikiwa. Zaidi linajengwa na timu, ndiyo maana litakuwa na
nafasi ya kufanya vema zaidi kwa kuwa iko makini.
Diamond
Platnumz, anaweza kuendelea kudumu kama Championi kama angekuwa
ametanguliza umakini na ikiwezekana angependa kuumiza akili yake zaidi
na mwisho, asianze kuamini Watanzania wengi ni wajinga na hawajui
kabisa.
GARI; DIAMOND |
GARI LIL WAYNE |
Juhudi
za Diamond ambaye alikulia katika maisha ya shida kutoka katika
Kitongoji cha Tandale katika Jiji la Dar es Salaam, zinapaswa kupewa
sifa na kuthaminiwa kwa kuwa zinasaidia vijana wengi kutaka kukua zaidi.
Lakini
kadiri siku zinavyosonga mbele, inaonekana hivi; Diamond amekwama
kiakili, timu inayomuongoza imekwama pia na inawezekana ina watu
walioridhika, wanaoamini wamefika au wanafikiri, hakuna anayeweza
kumfikia tena Diamond kwa kuwa hakuna kama yeye.
Wanawaza
hivyo kwa kuwa wamesahau mengi yaliyopita, kwamba hakuna shoo
zilizokuwa zinajaza kama za 2 Proud au Mr II au Sugu. Baadaye ikawa
hakuna kama Profesa Jay, Juma Nature, Lady Jaydee na wengine kama
makundi ya East Coast, Wanaume TMK na kadhalika lakini sasa wanaonekana
ni wa kawaida kabisa.
Huenda
wale wana makosa yao, lakini kosa kubwa la Diamond linataka kulingana
kabisa na vifo vya bendi za dansi ambazo zilikubaliana na kuamua kuiga
kila kitu cha bendi za DR Congo na baada ya hapo zikataka kushindana
sokoni na Wakongo.
ANARUKA DIAMOND... |
ANARUKA LIL WAYNE |
Leo
unamuona Koffi Olomide ambaye Muumini Mwinjuma alimkuta sokoni,
amemuacha na Mwinjuma kuinuka inaonekana ni hadithi itakayokuwa haina
mhadithiaji.
Kwa
nini inakuwa hivyo, ni kwa kuwa aliyeanza chake, mara zote anakuwa bora
zaidi kuliko anayeiga na tabia ya watu ni kupenda vilivyo bora hasa kwa
vile vinavyokuwa vimeanzishwa.
Mafanikio
ya kibiashara ni ubunifu mpya kwa kuwa macho na masikio ya mwanadamu
huvutiwa na kuona au kusikia mambo mapya na si kurudia na hasa
inapozungumziwa ubunifu.
DIAMOND AMETUPA FEDHA, WASIOCHANA WALIOKUWA KANDO YA BARABARA WANAGOMBEA |
LIL WAYNE AMETUPA FEDHA, WASIOCHANA WALIOKUWA KANDO YA BARABARA WANAGOMBEA |
Kuona,
kusikia na kuamini Diamond amekopi halafu akapesti na akarudia mara
nyingine ndani ya mwaka mmoja zaidi ya mara tatu, ni kujinyonga kwa njia
ya mkato na kutengeneza mwisho wake ingawa yeye anaamini haitatokea.
Diamond
Platnumz alimshirikisha AKA wa Afrika Kusini katika Wimbo wa Make Me
Sing, ulipotoka watu wengi badala ya kujadili ubora wa wimbo wenyewe,
suala la kuiga Wimbo wa Got Money ya Lil Wayne ndiyo likawa mjadala kwa
kuwa ilikuwa ni copy & paste bila ya aibu hata kidogo!
Wakati
Diamond anatoa wimbo wake, tayari huo wa Lil Wayne ulikuwa umetazamwa
na watu milioni 57. Wake ndani ya wiki chache ukawa umetazamwa na watu
zaidi ya 600,000. Hapa utajifunza ubora wa usahihi, lakini jiulize hao
milioni 57, wangapi waliingia katika 600,000 ya Diamond na wataweza vipi
kukichukulia ni kitu kipya na wanapaswa kufurahia.
WANENGUAJI WA DIAMOND |
WANENGUAJI WA TAYLOR SWIFT |
Tena
unaona Video ya Got Money ilitoka mwaka 2008, ya Diamond ni miaka zaidi
ya mitano baadaye, huenda anadhani Watanzania ni mazumbukuku, hivyo
hawawezi kuwa wang’amuzi.
Suala
hilo la Diamond kukopi, liliandikwa na gazeti hili Februari 19, mwaka
huu kwa kichwa cha habari, “Sare-sare maua”, mwandishi akiwa ni Hans
Mloli. Diamond amekaa si zaidi ya mwaka, amerudia jambo kama hilo,
ambalo nalo mjadala wake ni “copy & paste”.
Safari
hii ‘kahamishiaa’ video kadhaa ndani ya video yake moja ya wimbo wa
Kidogo ambao ameshirikiana na P Square. Wimbo ni mpya, mzuri na gumzo
lakini video yake imerudi palepale, “ya kuiga”,
Kuiga
bila ya kuboresha ni uzembe wa kufikiri, kutojiamini na ikiwezekana
naweza kuiita udanganyifu au kuwapotezea watu muda kwa kuwa sina sababu
ya kuangalia video ya msanii wa Marekani, halafu nikirejea kuangalia ya
Diamond nayo iwe vilevile.
JASMINE V, KIPANDE CHAKE HIKI KIMEIGWA KWENYE WIMBO WA DIAMOND SEHEMU ALIYOIMBA PETER OKOYE WA P SQUARE, ANGALIA PICHA YA CHINI. |
Au
Diamond anaamini anavijua vitu vya Marekani yeye peke yake pamoja na
meneja wake, Babu Tale, Said Fela, Sallam Sharaff maarufu kam SK,
wengine wote hawajui au hawajawahi kuona, hivyo hawatang’amua hata
kidogo!
Maana
katika video ya Kidogo, ndani yake amechukua sehemu zinazofanana kabisa
kwa utengenezaji na matukio katika video za wasanii Tyga na Jasmine V.
Ameiga
mambo ya video ya Wimbo wa Right There ya Jasmine V, kafanya hivyo
kwenye For The Road ya Tyga na kinachoshangaza hadi kukaa na mbwa
mweupe, mavazi ya warembo ambayo ni rangi ya njano na bluu na hata
mshono.
Hii
unaona katika video yake ya Make Me Sing aliiga vitu kama mavazi, aina
ya gari, aina ya uvamizi, fedha kutupwa barabarani na wanaogombea ni
wasichana ili kuzuia gari la polisi. Unajiuliza, hivi Diamond na timu
yake hawana uwezo hata kidogo tu wa kufikiria? Wamechoka au ndiyo
wamefika mwisho? Au Diamond alifika hapo kwa nguvu zake na sasa alionao
ni wasio na mawazo sahihi na hajui wanamtumbukiza shimoni?
DIAMOND AKIWA KWENYE MAVAZI MEUPE, MBWA MWEUPE ALIYE KULIA KWAKE KAMA ALIVYOFANYA TYGA KWENYE VIDEO YAKE, ANGALIA PICHA YA CHINI! |
Mimi
najiuliza, hata kama wale wanamtumbukiza shimoni, yeye mwenyewe haoni au
hawezi kujiuliza kwamba mambo anayofanya yatamuangusha kwa kuwa kazi
zake zinavuka mipaka hivyo itafikia siku moja anachaguliwa kwenye tuzo
ya BET au nyinginezo halafu video yake iliyotazamwa na watu 600,000
inashindana na ile yenyewe iliyotazamwa mara milioni 57 na yeye akiwa
ameiga.
Vipi
Diamond wakati anaingia kimataifa zaidi ndiyo anashindwa kuwa mbunifu
zaidi? Anaiga vya wale anaokwenda kushindana nao badala ya kutengeneza
ladha mpya? Hata kama Watanzania hawajui kama anavyoamini, ataweza vipi
kushindana kimataifa kwa “copy & paste”, tena ya waziwazi na
inayoshangaza kama kweli walioamua walikuwa hawajachoka!
Kama
watu wanaamini Diamond ndiye bora kuliko wasanii wote kutokana na
mafanikio yake, je, wanaomfuatia wanaweza vipi kuiga anachofanya kama
mfano au changamoto kama atakuwa anaiga video ya msanii mwingine
akashindwa hata kubadili nguo, gari na aina ya kukaa?
MEMBA WA P SQUARE AKIWA KATIKA SEHEMU YA WIMBO WA DIAMOND AMBAO UMEKOPIWA KUTOKA KATIKA WIMBO WA MSANII TYGA HAPO CHINI! |
Mfano
huyu akiwa na mbwa mweupe, basi Diamond alishindwa hata kutafuta mbwa
mweusi ili kuwa kitu tofauti! Jiulize hata ukaaji na upande alivyokuwa
amekaa Tyga na Diamond alishindwa kubadili, jamani huyu ni Diamond
yuleyule? Au amekubali kutengeneza kifo chake kimuziki, mapema kabisa!
Siku
chache zilizopita, unamuona muigizaji maarufu wa Hollywood na duniani
kote Terrance Howard akiwa amekaa na simba. Halafu siku chache
zinazofuata, unamuona Diamond akiwa naye amekaa na simba kwa mkao uleule
akionyesha uvivu wa kufikiri kwa kiwango cha juu tena ajabu zaidi,
simba wakiwa wanatokea Afrika na kwenda kufanyiwa kazi Marekani kabla ya
Tanzania na yule anayetokea kwenye simba wengi anakubali kuiga
vilevile.
Nikajiuliza
tena, hivi, kuliko Diamond kukaa kwani angemshika simba akiwa amesimama
au anatembea, ugumu ungekuwa nini! Bado ingewezekana Diamond kutafuta
mnyama mwingine ili kuepuka kuendelea kuonekana ni aliyechoka.
Inawezekana
kabisa, mashabiki wa Diamond wameamua kuamini kila kitu chake ni bora
bila ya kuchunguza. Watanzania wote hawawezi kuwa na akili zinazolingana
na kwa utandawazi wa kiwango cha juu, dunia sasa ni kijiji. Taratibu
ataanza kupoteza mashabiki mmoja baada ya mwingine.
Akiendelea hivi, Diamond lazima akumbuke ‘atajiua’ mwenyewe kwa kuwa wako wengine ‘walijiua’ na leo wanasuasua kurejea kileleni.
TERRANCE NA SIMBA, DIAMOND NAYE AKAKOPI VILEVILE AKIWA NA SIMBA...!! |
Kwanza
ni lazima abadilike na kama ataendelea hivi, hakuna ubishi, atakwisha
na kumalizika kabisa kisanii na mwisho, itabaki stori. Inawezekana
anaona sawa kwa kuwa wengi waliopaswa kumkumbusha hasa wanaohusika na
sanaa kwenye vyombo vya habari hasa redio na runinga mbalimbali,
wamegeuka kuwa wapambe kwake na wanachofanya ni kufurahia kila
anachofanya na kusifia ili kuepuka kupoteza urafiki naye!
Mwisho,
Diamond anapaswa kukumbuka, miaka sita iliyopita, hakuwa maarufu alivyo
sasa na kuna wengine walikuwa wakitamba. Akiendelea hivi, miaka sita
ijayo Mwenyezi Mungu akimjaalia uzima, atakuwepo lakini wengine watakuwa
wakitamba zaidi yake kwa kuwa watapita katika mashimo ya udhaifu wake
wa kuamini Watanzania hawajui lolote, kumbe kuna wengi kwa wingi wanajua
mengi zaidi yake kuhusiana na muziki wa ndani na nje ulikotoka na
unapokwenda.
source..GAZETI
la Championi
0 comments:
Post a Comment