Na Waandishi Wetu/Uwazi KWELI kila kifo kina sauti yake! Siku tatu zimekatika tangu Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Damian Mtokambali Komba kufariki dunia kwa matatizo ya presha na kisukari, jipya limebainishwa na Gazeti la Uwazi.
ILIKUWA MAKABURINI
Jipya hilo ni kuibuliwa kwa mahojiano yaliyowahi kufanywa kati ya marehemu na gazeti ndugu na hili, Amani la Mei 2, 2011 kwenye Makaburi ya Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo marehemu alisema akifa angependa azikwe kifahari.
ILICHOAGIZA
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika kwenye mazishi ya msanii wa Kundi la Tanzania One Theatre (TOT), Fatuma Ally ‘Fatuma Dogodogo’, marehemu Komba alisema hatafurahi kule aendako endapo atazikwa kwenye kaburi lisilo na hadhi.
Alisema: “Ninaamini kaburi langu likijengwa katika muonekano mzuri itakuwa rahisi hata kwa watu watakaokuwa wanakuja kuniombea kuvutiwa kuliko kunifukia kawaida.“Kwa hiyo nasema siku mimi nikifa naomba kaburi langu lijengwe kwa marumaru na juu liwekewe kioo cha ‘kuslaidi’ ili hata mtu akitaka kuja kufanya ibada ya kuniombea, avute kioo kisha ashuke ngazi hadi kwenye jeneza langu, siyo kama hivi wanavyozikwa wengine.”
KWA MAANA HIYO BASI
Kwa kauli hiyo ya Komba, alimaanisha kaburi lake, licha ya kujengwa kwa marumaru kwa nje na kuwa na kioo cha kuslaidi juu, lakini alipenda kuwe na ngazi za kutoka juu hadi chini ambako kuna jeneza.
Kauli ya Komba iliendelea kumaanisha kwamba, alitaka jeneza lake lisifukiwe kwa juu na zege wala udongo ili iwe rahisi kwa mtu kufika chini kumwombea.
MTOTO WA MAREHEMU AISEMEA FAMILIA
Akizungumza na Uwazi baada ya kuulizwa kuhusu wosia huo wa baba yake, mtoto mmoja wa marehemu aliyesema si msemaji wa familia hiyo alisema kuwa, katika vikao vilivyokaa juzi Jumapili, familia iliamua kwamba itafanya lile linalowezekana katika kuuhifadhi mwili wa baba yake kwenye nyumba yake ya milele.
“Huo wosia unaosema wewe mwandishi sisi hatuujui ila mwili wa baba utahifadhiwa vizuri na kwa hadhi yake kama baba yetu na Mbunge wa Mbinga.
“Pia tutazingatia kuwa, baba alikuwa mtu wa watu achilia mbali wapiga kura wake. Kwa hiyo hatutamwangusha baba yetu katika kuuhifadhi mwili wake,” alisema mtoto huyo.
RATIBA YA MAZISHI
Mwili wa marehemu Komba ulitarajiwa kutolewa Hospitali ya Rufaa Lugalo, Dar na kulazwa nyumbani kwake, Mbezi Tangibovu, juzi ambapo ungelela hapo.Jana, mwili ulitarajiwa kupelekwa kuagwa katika Viwanja vya Karimjee, Dar na baadaye kusafirishwa kwenda Songea ambapo ungeagwa kwenye Uwanja wa Majimaji na baadaye kuelekea Kijiji cha Lituhi, Mbinga, Ruvuma kwa mazishi leo hii (kama watafika mapema).
Marehemu Komba alifariki dunia kwenye Hospitali ya TMJ, Dar baada ya kuzidiwa nyumbani kwake.
Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
Habari: Haruni Sanchawa, Chande Abdallah, Denis Mtima na Shani Ramadhani/amani
0 comments:
Post a Comment