Na Waandishi Wetu
DUNIA imekwisha jamani! Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Mabibo, Dar, Irene Said (15) ametekwa, amebakwa na kuuawa kikatili kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili huku ikidaiwa kuwa, kijana mmoja asiyejulikana alifika nyumbani kwao, Kigogo Luhanga na kutaka kiroba na mtu mmoja waongozane akabebe ndizi.
Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha sana, mama mdogo wa marehemu, Doto Lucas alisema:
“Siku ya tukio ambayo ni Alhamisi iliyopita (Machi 12), kijana mmoja ambaye hakuna aliyemfahamu alikuja hapa nyumbani na kumtaka mtu mmoja na kiroba ili akachukue ndizi ambazo kuna mtu aliagiza ziletwe.
“Marehemu ndiye aliyekuwa karibu akijisomea baada ya kutoka shuleni. Mtu mkubwa aliyekuwa nyumbani muda huo ni bibi wa marehemu ambaye ni mtu mzima hivyo alimwambia Irene aongozane na mtu huyo akachukue mzigo akijua uko jirani kwa mujibu wa mtu huyo.
“Baada ya muda, yule kijana alirudi akiwa
peke yake na kusema anataka chombo kingine cha kubebea kwa kuwa kile
kiroba kilikuwa hakitoshi.“Bibi mtu alimuonesha ndoo kwa vile hakukuwa
na kiroba kingine, alipoitwaa na kuondoka nayo ndiyo hakurudi yeye wala
Irene.Wanafunzi wenzake wakiwa na majonzi msibani.
“Baada ya kuona muda unayoyoma bibi wa marehemu alianza kupata
wasiwasi. Ndipo akatutaarifu kilichotokea nyumbani na sisi tukaanza
kumsaka Irene na kijana yule.”KWA NINI WALIMWAMINI KIJANA HUYO?
“Sisi tuna makaka zetu wakubwa ambao wana kawaida ya kutuagizia mizigo mbalimbali kwenye magari, kwa hiyo tuliamini ni wao. Lakini tulipowapigia simu na kuwaeleza tukio hilo wote walikanusha kuwa si wao na kushangaa.
“Kauli hiyo ilianza kututia shaka zaidi hivyo tulianza kuwasiliana na ndugu na jamaa ambao wote waliishia kushangaa. Tukaenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi, Kigogo na kuanza msako wa kumsaka binti yetu pamoja na mtuhumiwa.”
IRENE APATIKANA AKIWA AMEUAWA
Mwanamke huyo anaendelea kusimulia: “Kesho yake asubuhi (Ijumaa) tukasikia kuna binti amekutwa ameuawa kinyama kwenye Bonde la Mto Msimbazi, eneo la Sukita. Tulipatwa na mshituko, tukaenda na kuukuta mwili, tulipoukagua tuligundua ni Irene.
“Alikuwa ameharibiwa vibaya. Sehemu za mwii alikuwa na damu, alichomwa na kitu chenye ncha kali. Kwa vyovyote yule kijana alikuwa na wenzake, walimteka huko mbele ya safari na kumbaka kabla ya kumuua. Inauma sana jamani.”
Marehemu Irene ambaye katika mazishi yake wanafunzi wenzake walikuwa wakilia sana, alizikwa Jumamosi iliyopita katika Makaburi ya Mburahati, Dar.
Katika ibada hiyo, Katekista aliyesaidiana na paroko kuendesha ibada hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Henjewele aliwalaani vikali walioshiriki kufanya unyama huo na kuwataka wafanye toba haraka iwezekanavyo na kumrudia Mungu wao vinginevyo laana na moto wa milele utawaangukia.
Mungu ailaze roho ya marehemu Irene mahali pema peponi- Amina.
Imeandikwa na Richard Bukos, Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa.
0 comments:
Post a Comment