Maelezo ya Ndugu Zitto Kabwe aliyoyatoa katika Mkutano na Waandishi wa Habari kufuatia Kung’atuka Ubunge na Kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo
Jumapili, 22 Machi 2015, Serena Hoteli, Dar es Salaam
Ndugu Waandishi wa habari, wanachama na wapenzi wa ACT-Wazalendo na wote mliohudhuria mkutano huu,
Kama mnavyojua siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu ya mwisho kuhudhuria bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma. Baada ya kung’atuka ubunge kufuatia kukoma uanachama wangu wa chama nilichotumia kuingia Bungeni, wengi mliniuliza ‘what is next?’
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi 2015 nilijiunga rasmi na Chama cha ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa ni moja kati ya siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya kisiasa. Na kwa leo kwa kweli nisingependa nizungumzie mgogoro uliokuwepo kati yangu na viongozi wangu wa chama cha zamani wala kile kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua, yameandikwa sana na yameshapita. Sasa ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame Nkrumah alipata kusema "forward ever, backward never". Na kama nilivyosema Bungeni, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kwa hiyo leo nitazungumzia uanachama wangu katika chama changu kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini nijiunge na chama kipya ambacho kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine wanachama wake bado wanajaa katika kiganja cha mkono?
Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii. Uadilifu ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa utumishi wa umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi kumi ya ACT-Wazalendo, uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi hiyo. Uwazi ni sehemu ya jina la chama hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba sitojiona mgeni katika chama hiki. Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na katika utumishi wa umma.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo. Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika kuondoa umaskini.
Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu, afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu yake.
Mwezi Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alipokea maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu. Maandamano yale yalichochewa na kasi kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya viongozi (wabenzi). Mwalimu alifoka kwa kuuliza “ Tunajenga nchi ya namna gani”? Hatimaye Azimio la Arusha likatangazwa.
Chama hiki kipya kimeanzishwa katika mazingira yale yale ya mwaka 1966. Ni wakati wa kujiuliza na kupata majawabu ya aina ya nchi tunayojenga. Sisi ACT – Wazalendo tumeona jawabu ni kurudi kwenye misingi. Waingereza wanasema ‘back to the future’ Let the new beginning begin.
Ahsante sana kwa kunisikiliza. Zitto Zubeir Kabwe Dar es Salaam, 22 Machi 2015.
0 comments:
Post a Comment