Muziki,Habari motomoto,MICHEZO,Maajabu,Picha Picha na mambo mengine mengi hapa ndani ya KALI ZA DJ YEYO

nongona

tangazo eligod

tangazo eligod

About the Author

CHECK me!!!!

CHECK me!!!!

Sunday, October 19, 2014

MAFUNZO ( 20) KUTOKA KWA ALIYEKUWA NGULI WA MUZIKI WA ZAMANI,KATIKA BAND YA MSONDO NGOMA.. TX MOSHI WILLIAM


KUNA makala ambazo huwa hazifi wala hazipotezi mwelekeo miaka na miaka, hii ni moja wapo. Makala hii iliandikwa mwaka 2008 na mwandishi mahiri wa burudani IBRAHIM MKAMBA, ikachapishwa na gazeti la Raia Mwema toleo namba 023 tarehe 2 April 2008. Hebu tiririka nayo.
JUMAMOSI iliyopita, yaani Machi 29, 2008, ilitimia miaka miwili kamili tangu mwanamuziki mahiri nchini, TX Moshi William wa Msondo Ngoma Music Band, afariki dunia baada ya kuuguza mguu kwa muda mrefu kufuatia ajali ya gari iliyotokea mwishoni mwa mwaka 2004.
Mengi yameandikwa na kutangazwa kuhusu maisha ya mwanamuziki huyo nguli katika uimbaji na utunzi wa nyimbo. Hivyo basi, katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kifo chake, nimeona ni vizuri tuangalie kitu tofauti kuhusiana naye kwa kutazama wasifu wake katika mambo 20 ya kuigwa na wanamuziki wengine. Mambo hayo ni:-
1. Kutobadili bendi bila sababu ya msingi
TX Moshi William ametufundisha kwamba maendeleo ya mwanamuziki kimaisha yanapatikana si kwa kuhama hama bendi.
Tangu mwanamuziki huyo alipotoka Polisi Jazz Band, Wana Vangavanga, mwaka 1982 na kujiunga na Msondo Ngoma, hakuhama bendi hiyo hadi alipofariki dunia lakini ameweza kujenga nyumba mbili na kumiliki gari na mali nyingine za thamani.
Kuna wanamuziki wamezunguka bendi kwa walichoeleza kutafuta maslahi lakini hawakufanikiwa kimaisha kama ilivyokuwa kwa marehemu TX Moshi William ambaye hakuhama bendi kwa miaka 24!  Funzo tunalopata hapa ni kwamba mafanikio ya mwanamuziki hayaletwi na kuhama hama bendi bali yanaletwa na kupangilia vizuri mambo yake popote alipo.
2. Waimbaji wajifunze kupiga vyombo
TX Moshi William alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga solo gitaa lakini aliamua kuwa mwimbaji. Funzo tunalopata hapa ni kwamba mwanamuziki aliyekamilika ni yule anayepiga angalau chombo kimoja cha muziki pia, siyo kuimba peke yake.
3. Tungo ziwe nzuri
Kuhusu hilo, TX Moshi William ametufundisha kwamba tungo iliyokamilika ni ile inayoimbwa kwa Kiimbo (melody) kizuri, yenye ujumbe makini wowote ule na yenye mapigo ya kuvutia ya vyombo, mambo ambayo yalikuwa dhahiri katika tungo zake zote zisizopungua 60 alizotunga.
Katika zote, hakuna sifa iliyokosekana katika sifa hizo.
4. Mafanikio ya bendi ndilo liwe lengo
Marehemu TX Moshi William aliweka mafanikio ya bendi mbele ya sifa yake binafsi. Kwa mfano katika wimbo kama  "Wanangu Nawausia" wa mwaka 1984 (...msiibe, msiue, msinyang'anye mali za watu, ni hatari kwa maisha) na "Kimanzichana" wa mwaka 1998 hakuimbisha popote ingawa alizitunga yeye.
Kwa "Wanangu Nawausia" alimuachia Fresh Jumbe ambapo kwenye "Kimanzichana" aliwaachia Muhidin Gurumo na Marehemu Joseph Lusungu. Hii ni mifano tu kati ya nyimbo nyingi alizofanya hivyo kwa manufaa ya bendi. Angekuwa mtu wa kujali sifa binafsi, asingeacha kuimbisha mwenyewe.
5.  Heshima kwa wanamuziki wengine na kwa mashabiki
Marehemu TX Moshi William aliwaheshimu sana wanamuziki wenzake, si wa bendi yake tu bali pia wa bendi nyingine na alifanya hivyo pia kwa mashabiki wa bendi yake.
Alifanya hivyo bila kujali jina kubwa alilokuwa Nalo kimuziki. Hili linafaa kutekelezwa na wanamuziki wetu chipukizi ambao wengi wao wakishaimba (nasisitiza wakishaimba)  wimbo mmoja tu na ukapendwa, wanajiona watu tofauti kabisa bila ya kuelewa kwamba hadhi yao inapandishwa na hao hao anaowadharau.
6. Tungo zijadili mambo tofauti tofauti
Katika tungo zake, Marehemu TX Moshi William amezungumzia mambo mengi tofauti kama kuthamini watoto (Mama Kanitupa), kutotelekeza na kujali familia(Baba Mai, Asha Mwana Seif), kujiepusha na vitendo vya uhalifu (Tahadhari, Wanangu Nawausia), hisia kali za mapenzi (Bahati) na udanganyifu kwenye mapenzi (Binti Maringo, Tuma na Gloria).
Vile vile, amezungumzia mtu kujali usalama wake (Nyabasi Mwana Ngoreme), mila na masuala ya kijamii (Queen Kase, Demokrasia ya Mapenzi, Kilio cha Mtu Mzima) na kujiepusha na ufujaji wa pesa (Tupatupa).
Haya ni maeneo machache kati ya mengi aliyoyagusa Marehemu TX Moshi William katika tungo zake. Watunzi wa sasa inabidi watambe kwenye eneo pana la masuala ya kuiasa jamii kama alivyofanya TX Moshi William badala ya kujikita kwenye hisia kali za mapenzi na kusutana tu.
7. Tungo mpya zizizidi za zamani kwa ubora.
Katika tungo za Marehemu TX Moshi William, kila tungo mpya zilikuwa bora zaidi ya za zamani. Hilo linafaa liigwe na watunzi wa leo ili kuonyesha mwanamuziki anapanda na siyo anashuka au kubaki palepale.
8. Unapohama bendi waachie wenzako nyimbo ulizotunga
Pamoja na kutunga nyimbo nzuri akiwa na Polisi Jazz, TX Moshi William hakuhama na wimbo wowote wa bendi yake hiyo ya zamani. Hakupeleka wimbo wa bendi hiyo Msondo wala Bana Mwambe, bendi yake ya "zing zong".
Huu ni ukomavu mkubwa kisanii na unaonyesha jinsi mtunzi makini anavyoangalia mbele kuandaa "vitu" bora kuliko vya awali.
9. Kubali vipaji vya wengine
Katika mahojiano kadhaa, nilimsikia na kumuona TX Moshi William akiwasifu baadhi ya wanamuziki vijana kwa kazi nzuri kama mtunzi wa wimbo "Nakuhitaji" (Caz-T), Twanga Pepeta na pia aliwasifu sana wakongo wa bendi za hapa na kusema wamewazidi Watanzania kimuziki.
Kukubali vipaji vya wengine ni ukomavu kisanii badala ya kuponda kwa wivu usio na maana.
10. Kutoiga muziki wa kikongo
Pamoja na kukubali kwamba Wakongo wako juu kimuziki, Marehemu TX Moshi William hakuiga hata kidogo muziki wa kikongo. Alisaidia sana kulinda uhai wa mapigo ya kwetu kwenye muziki.
11. Wanamuziki wawe watanashati na walimbwende
Hakuna ubishi kwamba marehemu TX Moshi William alikuwa mtanashati siku zote. Hii ilimjengea heshima yeye binafsi. Kama wanamuziki wote wa kiume watakuwa watanashati na wa kike walimbwende, kazi hii itapewa heshima inayostahili. Wanamuziki kujiweka wachafu wachafu kunasababisha kazi hii ionekane ya kihuni.
12. Wanamuziki wachangamke jukwaani
Marehemu TX Moshi William alikuwa anajituma sana jukwaani pamoja na wenzake kina Roman Mng'ande (Romario). Kuzubaa jukwaani kunashusha thamani ya nyimbo zinazopigwa.
13. Kuwa na hoja nzito unapohojiwa
Sifa mojawapo kubwa aliyokuwa nayo TX Moshi William ni kuwa na hoja nzito na za kuvutia kila alipohojiwa. Baadhi ya wanamuziki nchini wanaikosa sifa hii muhimu. Ni vizuri hili lirekebishwe kwa heshima ya fani hii.
14. Kutokuwa na tamaa ya uongozi
Licha ya mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya bendi yake, TX Moshi William hakuwa na tamaa ya kuwa kiongozi wa bendi. Mchango wake mkubwa kwa bendi ulikuwa dhahiri. Kwa mfano, katika nyimbo nane walizorekodi RTD (sasa TBC Taifa) mwaka 1989, yeye alitunga sita- "Queen Kase", "Nyabasi", "Tahadhari", "Baba Mai", "Belinda" na "Mkutano wa Zanzibar wa Umoja Wafanyakazi".
Hii ni robo tatu au asilimia 75 ya nyimbo walizorekodi mwaka huo. Marehemu Joseph Lusungu alitunga wimbo mmoja,"Mwanaenzi" na Marehemu Suleiman Mbwembwe alitunga mmoja pia, "Penye Penzi Hapakosi Tenzi".
Jitihada za kutaka uongozi wa bendi, husababisha majungu na mshikamano wa wanamuziki kuvunjika. Marehemu TX Moshi William aliepusha hilo.
15. Kutojenga chuki na wanamuziki wa bendi hasimu
Pamoja na upinzani mkubwa uliopo baina ya Msondo na Sikinde, Marehemu TX Moshi William hakuwahi kutamka wala kuonyesha kuwa alikuwa na chuki na mwanamuziki yeyote wa Sikinde.
Mmoja wa marafiki zake wakubwa alikuwa Shaaban Dede wa Sikinde waliyekuwa wakitambiana kirafiki kuhusu ubora wa bendi zao na ubora wa timu zao walizoshabikia. Marehemu TX Moshi William alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga wakati Dede ni Simba damu.
16. Kuwa tayari kupokea ushauri wowote wa kufaa
Akiwasifu Wakongo kwa kuwa juu kimuziki, Marehemu TX Moshi William alisema kuwa hao jamaa wakikupa ushauri fulani, ukiufanyia kazi, unajikuta unapata kitu kikubwa kipya kimuziki.
Kauli hiyo inaonyesha alikuwa akitafuta, akipokea na kuufanyia kazi ushauri wa wengine badala ya kujiona ameshafika kwenye kilele cha mafanikio.
Wanamuziki wengine wanapaswa kuiga utaratibu huo kwa maendeleo yao.
17. Kuwa na moyo wa kufundisha wengine
Marehemu TX Moshi William anakumbukwa sana kwa jinsi alivyowasaidia baadhi ya wanamuziki wachanga kuinuka. Hakuwa na choyo katika hilo, kitu ambacho wataalam wa leo wanapaswa kufanya kwa wanamuziki wachanga.
18. Kuishi katika uadilifu
Marehemu TX Moshi William alikuwa mwadilifu, ikithibitishwa na juhudi alizofanya kurudisha zawadi aliyopewa na uongozi wa TOT Plus Band ili ajiunge nao.
Alipohisi asingeweza kuiacha Msondo, alifanya juhudi kurudisha, bila vuta nikuvute zawadi yote aliyopokea na kubaki na Msondo yake.
19. Kupenda na kuthamini kazi zetu
Marehemu TX Moshi William aliipenda na kuithamini kazi yake kiasi cha kuifanya hata alipokuwa akiugua. Wengi wetu hutoa visingizio ili tuwe nje ya kazi zetu, jambo ambalo ni kinyume cha alivyofanya TX Moshi William.
20. Kuwatengenezea wategemezi wetu maisha mazuri ya baadaye.
Ni vizuri wanamuziki wakaishi kama alivyoishi marehemu TX Moshi William kwa kutengeneza marafiki wengi na kupunguza sana maadui. Maisha ya aina hiyo ya TX Moshi William ndiyo yanayofanya wanafamilia yake aliowaacha wapate msaada na ushirikiano kutoka kwa washirika wake.
Angeishi maisha ya kujenga maadui wengi na ya kujitenga, leo hii wanafamilia yake aliowaacha wangekosa ushirikiano wanaoupata.
Wanamuziki wote wazingatie mafunzo hayo 20 kutoka kwa Marehemu TX Moshi William.
Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema Moshi William, mpenda wote aliyetutoka Machi 29,2006. Amen.

0 comments: