SERIKALI
imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53,
ambayo nguvu kubwa imewekwa katika kukusanya mapato kwa kulinda viwanda
vya ndani na kubana matumizi ya serikali ili kuelekeza sehemu kubwa ya
matumizi katika maeneo ya vipaumbele.
Katika
bajeti hiyo, bidhaa za lazima zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo
mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru wa barabara na maji ya
kunywa, havijaguswa huku bidhaa za starehe kama bia, sigara, soda, juisi
na nyingine kama nguo za mitumba, huduma za kupanga nyumba na
uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa kodi, huku kiinua mgongo cha
wabunge, kufutiwa msamaha wa kodi.
Aidha,
makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ikiwemo mapato ya taasisi za
udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Mafuta (EWURA),
Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine
za udhibiti, sasa yatapelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa
Serikali ambapo mahitaji yao ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na
Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa ya mapato waliyokusanya.
Aidha,
maduka ya kutoa huduma katika majeshi, yamefutiwa kodi rasmi na badala
yake, Serikali inajipanga kuongeza posho kwa askari, ili iwasaidie
kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na ofisi zote za Serikali,
zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni asiyetumia mashine za
kodi za kielektroniki (EFD’s).
Kodi juu
Katika
bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi ni pamoja na vinywaji baridi,
kutoka Sh 55 kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa forodha katika maji ya
matunda (juisi) yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa nchini,
ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka 11 kwa lita. Juisi zinazotokana na
matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru wake pia umepanda kutoka
Sh 200 kwa lita hadi Sh 210 kwa lita.
Bia, vilevi, mvinyo
Kwa
upande wa bia, serikali imependekeza bia inayotokana na nafaka ya hapa
nchini, ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru upande kutoka Sh 409 kwa
lita mpaka 430.
Bia
zingine, ushuru wake pia umepanda ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729
kwa lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni pamoja na vinywaji vya
kuongeza nguvu, ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita mpaka Sh 534.
Kwa
upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu zilizolimwa nchini kwa
kiwango cha asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka Sh 192 kwa lita
mpaka Sh 202.
Ushuru
wa mvinyo unaotengenezwa na zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango
kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali, havikuachwa nyuma maana ushuru umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.
Sigara
Sigara
zisizo na kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya hapa nchini kwa
kiwango angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi Sh 11, 854 kwa kila
sigara 1,000.
Kwa
upande wa sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini
kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa
kila sigara 1,000.
Sigara
zenye sifa tofauti na hizo, ambazo hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya
ndani, ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285 hadi Sh 50,700 kwa kila
sigara 1,000.
Katika
tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa kuwa sigara, ushuru wake
umeongezeka kutoka Sh 24,388 hadi Sh 25,608 kwa kilo huku ushuru wa
sigara aina ya Sigar ukibaki kuwa asilimia 30.
Vilainishi, gesi asilia, simu juu
Katika
mafuta ya kulainisha mitambo, ushuru umepanda kutoka Sh 665.50 kwa lita
hadi Sh 699 kwa lita, huku ushuru wa grisi za kulainisha mitambo,
ukipanda kutoka senti 75 kwa kilo, hadi senti 79 kwa kilo.
Gesi asilia pia ushuru umepanda kutoka senti 43 kwa futi za ujazo mpaka senti 45 kwa futi za ujazo.
Kuhusu
viwango vya ushuru wa kuhamisha fedha kwa kutumia simu, serikali
imependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10, kwenye ada zinazotozwa na
watoa huduma wa simu, katika kutuma na kupokea fedha, badala ya ushuru
huo kutozwa tu katika kutoa fedha.
Kwa
mujibu wa Dk Mpango, kwa utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa
huduma zimetumia mwanya wa kuhamisha sehemu kubwa ya ada hizo kwenye
kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.
Ulaji wa wabunge, hisa
Kwa
upande wa kiinua mgongo cha wabunge wakati wa kustaafu, sasa kitatozwa
kodi kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa
na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa.
Aidha,
mapato yote yatokanayo na hisa katika kampuni mbalimbali sasa yatatozwa
kodi, baada ya kufutwa kwa msamaha kwa waliokuwa wakimiliki hisa chini
ya asilimia 25.
Kodi ya mishahara
Katika
kodi inayokatwa katika mishahara (P.A.Y.E), imepunguzwa kutoka asilimia
11 mpaka tisa kwa wafanyakazi wanaopata mshahara wa kuanzia Sh 170,000
lakini hauzidi 360,000. Kwa wanaopata zaidi ya 360,000 lakini haizidi
540,000, watakatwa Sh 17,100 pamoja na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi
Sh 360,000.
Kabla ya hapo walikuwa wakikatwa Sh 20,900 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.
Wanaopata
zaidi ya Sh 540,000 lakini haizidi Sh 720,000, watakatwa Sh 53,100
pamoja na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi 540,000.
Kabla
ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 56,900 na hiyo asilimia 25 ya kiasi
kilichozidi 540,000. Kwa wanaopata zaidi ya Sh 720,000 wao watakatwa Sh
98,100 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh 720,000.
Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 101,900 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kilichozidi Sh 720,000.
Kodi za nyumba
Serikali
pia imependekeza malipo ya kupanga nyumba, nayo yatozwe kodi ambayo
haikuweka kiwango, ila imependekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato,
apewe mamlaka ya kukadiria kiwango cha chini na cha juu cha mapato
yapatikanayo na pango ili yatozwe kodi.
Kodi za nyumba, usajili magari, pikipiki
Mbali
na mapato ya kodi za nyumba, Serikali imependekeza kupandisha ushuru wa
kusajili magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa kila
gari na kutoka Sh 45,000 hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.
Kwa watumiaji wa namba binafsi za magari, ada sasa itapanda kutoka Sh milioni 5 kila baada ya miaka mitatu mpaka Sh milioni 10.
Kodi ya majengo
Aidha,
kodi za majengo sasa hazitakusanywa na halmashauri, badala yake TRA
ndiyo inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria, kukusanya, kuhifadhi na
kuiwakilisha katika halmashauri husika.
Mbali
na TRA kupewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, serikali pia
imependekeza kupunguza misamaha ya kodi za majengo ili majengo mengi
zaidi yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.
Ulindaji wa Viwanda
Saruji
aina ya (HS Code 2523.29.00) zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ushuru wake wa forodha umepandishwa kutoka asilimia 25 mpaka
asilimia 35 ili kulinda saruji inayozalishwa nchini dhidi ya ushindani
wa bei ya saruji kutoka nje ya nchi.
Kwa
bidhaa za chuma ikiwemo mabati kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki, nazo ushuru umetoka asilimia 0 mpaka 10, ili kulinda
uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini, huku bidhaa za nondo kutoka nje
nazo zikipandishwa kodi kutoka asilimia 10 mpaka 25, kwa nia ya kulinda
viwanda vya ndani.
Nyavu
za kuvua samaki kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushuru wake
umepanda kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 huku vichujia vya
vilainishi na petroli kutoka nje ya nchi vikiongezwa ushuru kufikia
asilimia 25 kutoka asilimia 10, ili kulinda bidhaa za ndani.
Sukari, ngano, mitumba, mafuta ya kula
Katika
sukari, serikali imekusudia kupunguza msamaha wa kodi na hivyo
waagizaji wa bidhaa za sukari kutoka nje watalazimika kuanza kulipa
ushuru wa asilimia 15 kutoka asilimia 10, huku ikitarajiwa kuongezeka
zaidi na kuwa asilimia 20 mwaka 2017/18 na asilimia 25 mwaka 2018.19,
ili kulinda viwanda vya ndani.
Kwa
upande wa ngano kutoka nje, ushuru umepunguzwa kutoka asilimia 35 mpaka
10, kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha
kulingana na mahitaji.
Kwa
upande wa nguo na viatu vya mitumba Serikali imepandisha ushuru kutoka
dola za Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4 kwa kilo, kwa nia ya
kudhibiti nguo hizo lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia uingizaji
wake.
Kwa
upande wa mafuta ya kula kutoka nje nayo ushuru umepanda kutoka
asilimia 0 mpaka 10 kwa mafuta ghafi ya kula, ili kuimarisha kilimo cha
mbegu za mafuta na viwanda vya ndani.
Tozo za pamba, kahawa, korosho
Miongoni
mwa tozo zilizofutwa kuondoa kero kwa wananchi ni mchango kwa kila
kiwanda cha kuchambua pamba wa Sh 450,000 na ada ya vikao vya
halmashauri wakati wa kujadili wafanyabiashara wa pamba ya Sh 250,000.
Kwa
upande wa kahawa, Serikali imefuta ada ya leseni ya kusindika kahawa ya
dola za Marekani 250, huku ushuru wa kusafirisha korosho wa Sh 50 kwa
kilo, ukifutwa.
Tozo
zingine zilizofutwa katika korosho ni ushuru wa chama kikuu cha
ushirika Sh 20 kwa kilo, gharama za mtunza ghala Sh 10 kwa kilo, kikosi
kazi cha kufuatilia masuala mbalimbali Sh 10 na makato ya unyaufu.
Pia
Serikali imepanga kuendelea kufuta tozo nyingine zinazokatwa na
halmashauri, wakala na mashirika katika mazao ya wakulima, baada ya
kufanya tathmini za kina.
Maduka kambi za jeshi
Serikali
imependekeza kufuta msamaha wa kodi uliokuwa ukitolewa katika maduka na
migahawa maalumu kwa ajili ya askari wa majeshi, kutokana na msamaha
huo kutumiwa vibaya na kupoteza mapato ya serikali na badala yake,
askari watapata posho mpya juu ya posho ambazo wamekuwa wakipewa.
0 comments:
Post a Comment