TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kama
ambavyo imeripotiwa kwenye vyombo vya habari na njia zingine za
upashanaji habari tangu jana kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi
ya CHADEMA, Ndugu Saed Kubenea aliwekwa chini ya ulinzi na kuamriwa
kwenda kituo cha polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul
Makonda ambaye inadaiwa hakutaka mbunge huyo azungumze na wananchi ambao
ni Wafanyakazi wa Kiwanda cha Tanzania Took Garment, waliokuwa
wamemuita mbunge huyo kwa ajili ya kumweleza matatizo wanayokumbana nayo
kazini hapo, ikiwa ni pamoja na ujira kidogo na mazingira magumu ya
kazi.
Aidha
akitambua kuwa alichofanya matumizi mabaya ya dhamana ya uongozi, hivyo
akakusudia kuficha umma usijue uovu huo, katika tukio hilo Makonda
aliwaagiza polisi wakamate kamera za waandishi wa habari waliokuwa
katika eneo hilo wakitimiza wajibu wao wa kikazi na kitaaluma kwa jamii.
Katika hatua ya sasa, tunaomba kusema ifuatavyo;
1.
Tukitambua kuwa mamlaka ya DC kuamuru watu kukamatwa yamefafanuliwa
kisheria na kuwekewa mipaka yake ambayo Makonda amedhihirisha kuivuka
katika nyakati tofauti sasa, Mkuu huyo wa wilaya hana mamlaka ya
kisheria wala ya kisiasa kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge,
tena aliyekuwa anatekeleza wajibu wake, tunamtaka DC Makonda amwachie
Ndugu Kubenea mara moja huku tukitoa wito kwa mamlaka zilizomteua
kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za kuwa kiongozi wa ngazi
hiyo.
2.
Kwa kuwa amri hiyo si halali kwa sababu haina msingi wowote wa
kisheria, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kumuachia Ndugu Kubenea ili
aendelee na uhuru wake huku akitekeleza wajibu wake wa kuwawakilisha
wananchi wa Ubungo badala ya kumsumbua kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.
3.
Halikadhalika, Jeshi hilo liwarudishie waandishi wa habari vifaa vyao
vya kazi vikiwa katika hali salama na bila athari yoyote ama ya vifaa
vyenyewe au materials yaliyoko ndani yake.
4.
Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoa kauli ya kuwahakikishia usalama
waandishi wa habari na vifaa vyao kila wanapotimiza wajibu wao kwenye
matukio yanayomhusisha Makonda kwa sababu tayari ushahidi unaonesha
anaweza kuwa tishio kwao binafsi na vitendea kazi vyao hususan pia
wanapokuwepo polisi.
5.
Kwa kitendo cha DC Makonda kuamuru kiongozi wa wananchi akamatwe bila
kuwepo kosa lolote la kisheria, CHADEMA tutachukua hatua za kisheria
dhidi ya DC huyo ili liwe fundisho kwake mwenyewe, wakuu wa wilaya
wengine na utawala mzima wa Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli,
ili watambue kuwa suala la kuongoza nchi kwa kuzingatia Haki, Katiba,
Sheria na taratibu si suala la kupenda bali ni lazima kuzingatiwa kwa
ajili ya amani na utulivu wa kweli.
Tutachukua
hatua hizo huku tayari kukiwa na kumbukumbu za Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora (THBU) ambayo hivi karibuni ilimuonya DC Makonda na
wakuu wa wilaya wengine na wakuu wa mikoa ambao wameanza tabia ya
kuendesha nchi kwa amri ambazo hazina uhalali wowote zikiwa nje ya
mamlaka yao ya kisheria kufanya hivyo.
Tuliamini
angalizo hilo la THUB ambacho ni chombo huru cha serikali, lingeweza
kuwa mwongozo sahihi kwa viongozi wa serikali na kwamba kosa la awali la
Makonda kuwaweka mahabusu watumishi wa Wilaya ya Kinondoni walioko
chini yake lingechukuliwa kama fundisho kwake, lakini bahati mbaya
watawala wanaweka nta masikioni linapofika suala la haki za binadamu na
uongozi bora.
Imetolewa leo Jumanne, Nov. 15, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
CHADEMA
0 comments:
Post a Comment