Wimbo wa Komba wamliza Raisi Kikwete kwenye Msiba Stori nzima Hii hapa...
Dar es Salaam. Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi na
kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa
machozi ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na
kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais
Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge,
Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu
mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la “Nani Yule”
ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu
machozi iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha
na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo
hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu,
msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo ni King Kiki,
Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni mwanamuziki wa
bendi ya Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.
Wakati wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo huo, idadi ya watu
wanaolia ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu na jamaa wa
marehemu.
Waombolezaji walisikika wakilia huku wakisema, “Jamani alikuwa
akitunga nyimbo kuwaimbia wenzake waliofariki dunia, sasa leo anaimbiwa
yeye.”
Alipofariki Mwalimu Nyerere Oktoba 14, mwaka 1999, aliyekuwa Mbunge
wa Mbinga Magharibi, Komba akiwa na bendi ya TOT alitunga nyimbo za
maombolezo ukiwamo wa “Nani Yule’, ‘Kwaheri Mwalimu’, ambazo jana
zilitumiwa na wanamuziki kumuimbia yeye, wakibadilisha baadhi ya maneno.
Mwili wa mbunge huyo (61) aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita kwa
ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, uliagwa katika viwanja vya
Karimjee ambapo salamu mbalimbali za rambirambi zilitolewa kabla ya
mwili huo kusafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Hata wakati wa kuagwa mwili huo, idadi kubwa ya wabunge wenzake
waliohudhuria walishindwa kujizuia kulia huku wakikumbushana ucheshi
aliokuwa nao Komba enzi za uhai wake.
Pengine msiba huo utakuwa umewagusa wengi wanaomfahamu kwa mambo
mengi, na kwa kuwa kipindi hiki nchi inajiandaa kupata rais mpya, kwa
kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ni kuipigia debe CCM kupitia uimbaji wake.
Kulingana na maelezo ya waombolezaji, Mwanajeshi huyo aliyestaafu
akiwa na cheo cha kapteni alikuwa ni mtu ambaye hakusita kueleza kile
alichokiamini, jasiri asiyekubali kushindwa, mcheshi wakati fulani na
mtu wa kutoa misaada.
crdt mwananchi
0 comments:
Post a Comment