Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge limepitisha azimio la kuwasimamisha kuhudhuria vikao
vya Bunge baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliohusika katika
kufanya vitendo vya vurugu ndani ya ukumbi na kudharau Mamlaka ya Spika
Januari, 27, 2016.
Wabunge
waliosimamishwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mhe.Kabwe Zubeiri Ruyangwa
Kabwe, Mhe.John Heche, Mhe.Halima Mdee,Mhe.Tundu Lissu, Mhe.Halima Mdee,
Mhe.Pauline Gekul na Mhe. Ester Bulaya.
Azimio
la adhabu kwa wabunge hao limetolewa na Bunge chini ya Kifungu cha 30A
(1) cha sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na kanuni
ya 74 (4) na (6).
Akisoma
adhabu hizo Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe 15 Mhe.George
Huruma Mkuchika amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati hiyo kwa
kuwaita na kuwahoji wahusika ulibaini kuwa wabunge hao walitenda kosa
kwa kukiuka kanuni zinazoliongoza bunge hilo.
Imebainishwa
kuwa Mhe.Zitto Kabwe alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e)
cha Sheria ya Haki na Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni
ya 60(2) na (12) , 74(1) na (b) kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata
utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.
Kamati
hiyo ilibaini kuwa Mhe.Godbless Lema, Mbunge wa Arusha alivunja
Masharti ya kifungu cha 24 (c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge Sura ya 296 pamoja na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya
kanun hiyo Kudharau Mamlaka ya Spika.
Kwa
upande wa Mhe.John Heche alivunja kanuni ya 72 (1) na 68(10) ya kanuni
za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo
limekwishatolewa mwongozo na kuongeza kuwa vitendo hivyo vilivuruga
shughuli za Bunge.
Kwa
mujibu wa maelezo ya kamati hiyo Mhe.Halima Mdee, Mhe.Tundu Lissu,Mhe
Pauline Gekul na Mhe.Ester Bulaya walivunja masharti ya kifungu cha 24
(c), (d) na (e) cha sheria ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya
296 na Kanuni ya 72 (1)68 (10), 60(2) na 12 na 74(1) (a) na (b) kwa
kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa
uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.
Kufuatia
uchunguzi huo Bunge kupitia kamati hiyo limeazimia kuwa Mhe. Ester
Bulaya na Mhe.Tundu Lisu wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa
Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei , 2016 pamoja
na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa
walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa
kwa mamlaka ya Spika.
Aidha,
Bunge limeazimia kuwa Mhe. Pauline Gekul, Mhe.Godbless Lema, Mhe.Zitto
Kabwe na Mhe Halima Mdee wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa
Bunge kuanzia tarehe 30 Mei 2016.
Aidha
Bunge limeazimia Mhe.John Heche asihudhurie vikao kumi mfululizo vya
Mkutano wa Tatu wa Bunge hilo kuanzia Mei, 30, 2016 kwa kuwa alipatikana
na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati kwa kufika
na kujibu maswali yote kama alivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya
kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.
Pamoja
na adhabu hizo Kamati hiyo imetoa maoni na mapendekezo kuwa Bunge
liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu matumizi ya
uzingatiaji sahihi wa kanuni sahihi wa kanuni za Kudumu za Bunge hasa
kanuni za majadiliano ndani ya Bungeni.
Aidha,
Kamati hiyo imesema kuwa ipo haja ya kutungwa kwa kanuni za maadili kwa
wabunge wote kama kifungu cha 12 A Cha Sheria ya Kinga, Haki na
Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu kwa
wabunge kwa kuhakikisha heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.
Kwa
upande wao baadhi ya wabunge wakichangia kwa nyakati tofauti kuhusu
suala hilo wamesema kuwa ipo haja ya Bunge kurudisha heshima yake kwa
wabunge wote kuheshimiana na kutoa michango yenye staha kwa kuzingatia
nafasi walizonazo katika jamii.
Wamesema
kuwa michango wanayoitoa ndani ya Bunge hilo lazima ijikite katika
masuala yanayowahusu wananchi wanaowawakilisha badala ya mambo
yanayochochea vurugu na kulifanya Bunge lipoteze heshima yake katika
jamii.
Aidha,
wabunge hao wamekubali kwa kauli moja kuanza upya kuzingatia kanuni
zinazoendesha vikao vya Bunge huku wakimtaka Spika wa Bunge au Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutosita kuchukua hatua za haraka
kwa mbunge yeyote atakayekiuka utaratibu na kanuni zilizowekwa.
0 comments:
Post a Comment