Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amemtimua kazi mkandarasi
anayejenga mfereji wa Buguruni kwa Mnyamani, Manispaa ya Ilala kwa
kushindwa kuujenga kwa kiwango kinachotakiwa.
Mbali ya kuchukua hatua hiyo jana, pia Waziri Mhagama aliagiza mkandarasi huyo asilipwe chochote.
Akiwa
Tegeta, waziri huyo alimbana Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni,
Ando Mwankuga na kumpa saa sita ampelekee taarifa ya ujenzi wa mfereji
wa Tegeta – Basihaya uliojengwa chini ya kiwango.
Maeneo
hayo ni yale ambayo miezi saba iliyopita, Rais mstaafu Jakaya Kikwete
aliagiza ijengwe mifereji haraka ili kunusuru uhai wa wananchi waliokuwa
wanasumbuliwa na mafuriko ya mara kwa mara.
Machi
24, Kikwete aliagiza kuvunjwa kwa nyumba zilizojengwa juu ya karavati
lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa maeneo
hayo, agizo ambalo bado halijatekelezwa.
Mvua
iliyonyesha siku mbili zilizopita ilisababisha nyumba 200 za eneo la
Basihaya - Tegeta kukumbwa na mafuriko na nyingine 500 za eneo la
Buguruni kwa Mnyamani zikiwa hatarini.
Mafuriko
ya wakati huo yalitokana na mvua zilizonyesha kwa wiki mbili mfululizo
na kusababisha vifo vya watu 12 huku mamia wakikosa makazi yao. Kutokana
na hali hiyo, Mhagama aliagiza wahandisi waliosimamia mradi wa
Basihaya, kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria akiwaita ni
‘wahandisi mizigo’.
Akiwa
Buguruni kwa Mnyamani, Mhagama alishuhudia ujenzi wa mfereji wa maji
ulio chini ya kiwango huku ukiwa haujakamilika. Mfereji huo uliokuwa
ukitakiwa kukamilishwa kwa miezi mitatu tangu Mei, ungegharimu Sh300
milioni.
“Huu
ni utani wa maisha ya Watanzania. Imepita miezi mingi hapa katikati na
jua lilikuwa linawaka. Ina maana mkurugenzi na mkandarasi hamjawahi kuja
kuona nini kinaendelea? Naagiza huyu mtu asiendelee kujenga na wala
asilipwe hata shilingi mia moja. Kama mlishamlipa, fedha hizo mtaifidia
Serikali,” alisema Mhagama.
Aliwatahadharisha
kuwa ikiwa mvua zitanyesha na kusababisha maafa kwenye eneo hilo kabla
mfereji kukamilika, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Isaya Mungulumi
na Mhandisi wake, Jaffari Bwigane watawajibika.
Ikiwa
mfereji huo utajengwa kwa uhakika, utasaidia kunusuru watu zaidi ya
1,163 wa eneo hilo, kukumbwa na mafuriko kama kipindi kilichopita.
Katika
ufafanuzi wake, Mungulumi alisema walibaini kuwa mkandarasi huyo
ameshindwa kujenga kwa kiwango wiki mbili zilizopita na kwamba, tayari
walianza kumchukulia hatua.
Aliilalamikia
Sheria ya Ununuzi ya Umma kuwa ndiyo iliyowafanya kumpa muda wa wiki
mbili ajirekebishe kabla ya kumtimua kama ilivyofanyika. “Bado hatujamlipa kiasi chochote cha fedha kwa sababu mkataba wetu ni ujenzi kwanza, ndipo alipwe,” alisema.
Akiwa Tegeta Basihaya, Mhagama alisema: “Wahandisi
mizigo wanaoshindwa kusimamia miradi muhimu kama hii lazima wachukuliwe
hatua za kisheria. Wote wavunjaji wa sheria na wanaoshindwa kusimamia
sheria hawawezi kuendelea kuwa chanzo cha maafa kwa watu wengine.”
Alimtaka
Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Makonda kusimamia suala hilo ili kunusuru
maisha ya wananchi kwani nyumba 200 zimezingirwa na maji.
Alisema haiwezekani mvua ya saa chache ikasababisha mafuriko kwenye eneo ambalo tayari Kikwete alishatoa maelekezo.
Kikwete
aliagiza Manispaa ya Kinondoni kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye
mkondo wa maji katika eneo hilo, agizo ambalo halikutekelezwa. Kutokana
na hali hiyo, Mhagama aliagiza zibomolewe.
Makonda alikiri ujenzi huo kutokuwa wa kiwango: “Nashukuru
waziri umekuja, ni kweli wapo watendaji mizigo kwenye halmahauri yetu,
hasa hawa wasimamizi wa miradi kama hii inayojengwa kuokoa maisha ya
wananchi.”
Katika
taarifa aliyoitoa kwa Kikwete, Makonda alisema mradi huo ili ukamilike
ungehitaji zaidi ya Sh3 bilioni. Jana Diwani wa kata ya Kunduchi,
Michael Urio alisema kuwa Sh1.2 bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi
wa mradi huo ambao bado unahatarisha maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Kaimu Mkurugenzi, Mwankunga alisema upungufu uliojitokeza kwenye mradi huo utarekebishwa. “Kabla
ya saa kumi (jana) tutampelekea Waziri taarifa ya ujenzi wa mradi huu
kama alivyotuagiza. Kuhusu makandarasi mizigo tutachunguza ikiwa wapo
basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa,” alisema.
Injinia
wa umwagiliaji wa Manispaa hiyo, Fransis Mugisha alisema, hawezi
kueleza chochote kuhusu mradi huo licha ya kuwa ulijengwa kwa usimamizi
wa ofisi yake.
“Sina ‘comment’ kwa sababu waziri ameagiza na kama kuna wahandisi mizigo basi sheria ipo,” alisema.
Juzi,
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadick kuwa ili mradi huo unahitaji Sh6 bilioni.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu
wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), akimsikiliza mkazi wa
Tegeta, Basihaya Jijini Dar es Salaam, Jumanne Malongo alipokuwa
akimueleza jinsi wembamba wa mtaro huo unavyosababisha maji kujaa katika
makazi yao, jana wakati alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo
ilivyojiandaa kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo,
kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
Kaimu
Mkurugenzi Halmashauri ya Manisipaa kinondoni, Ando Mwakunga akimueleza
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana
na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), uharibifu wa
“kalvati” katika eneo la Boko, Ununio Jijini Dar es Salaam, jana wakati
Waziri huyo alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo ilivyojiandaa
kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo.
0 comments:
Post a Comment