MENEJA wa Chelsea Jose Mourinho amesema anahisi ‘kazi yake inasalitiwa’ mara baada ya Jana Usiku kuchapwa Bao 2-1 na Leicester City kwenye Mechi ya Ligi Kuu England.
Kipigo hicho kwa Chelsea ambao ni Mabingwa Watetezi ni cha 9 kwao katika Mechi 16 na kimeipa mwanya Leicester City kuongoza Ligi wakiwa Pointi 20 mbele ya Chelsea ambao wako Nafasi ya 16 wakiwa Pointi 1 tu juu ya zile Timu 3 za mkiani ambazo zipo eneo hatari la kuporomoka Daraja.
Akiongea mara baada ya kipigo hicho, Mourinho alisema: “Moja ya sifa zangu bora ni kuusoma Mchezo kwa ajili ya Wachezaji wangu na sasa nahisi kazi yangu inasalitiwa. Moja ya uwezekano ni kuwa Msimu uliopita nilifinya kazi nzuri sana na kuwafikisha Wachezaji eneo la juu ambalo si lao na hawawezi kulidumisha.”
Msimu uliopita ambao Chelsea walitwaa Ubingwa walifungwa Mechi 3 tu za Ligi na kutwaa Ubingwa wakiwa Pointi 8 mbele ya Manchester City.
Jumamosi ijayo Chelsea watakutana na Sunderland ambao wako Nafasi ya Pili toka mkiani.
Mourinho aliongeza: “Nakubali tupo eneo hatari la kushuka Daraja lakini sikubali tupo vita ya kushuka Daraja!”
“Kila Siku Mazoezini sina la kulaumu Wachezaji wangu. Lakini inasikitisha kuona wanachofanya Mazoezini na kile wanachofanya kwenye Mechi.”
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kumaliza 4 Bora na kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI, Mourinho alijibu: “Hatuwezi kumaliza 4 Bora lakini tunaweza kumaliza 6 Bora kwa vile Timu nyingi zinapoteza Pointi. Kwa sasa tupo eneo ambalo naona aibu!”
Kuhusu hali tete inayomkabili na nini hatima yake kuendelea kama Meneja, Mourinho alijibu: “Hili ni swali la kila siku. Kitu pekee ninachoweza kusema ni kuwa nataka niwe Meneja. Sina wasiwasi na siogopi changamoto kubwa na wakati huu hii ni changamoto kubwa sana. Nataka nibaki na natumai Bwana Roman Abramovich na Bodi inataka nibaki kwa sababu nataka kubaki!
0 comments:
Post a Comment