Jeshi la Polisi Mkoani hapa limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye
Ismail Swalehe Sang’wa (20) ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Sepuka
wilayani Ikungi katika Mkoa wa Singida kwa tuhuma za kumuua Afisa wa
Intelijensia wa TANAPA aitwaye Emily Kisamo (52).
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana asubuhi , Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema
tukio hilo la mauaji ya Afisa huyo wa TANAPA lilitokea tarehe 18.12.2015
muda kati ya saa 2:30 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi mtaa uitwao
Corridor Area Uzunguni jijini Arusha.
Kamanda
Sabas alisema
kwamba, siku ya tukio hilo marehemu alikuwa nyumbani kwake sebuleni
akiwa anakunywa uji ndipo mtuhumiwa ambaye ni mfanyakazi wake wa ndani
alimvizia na kumkata shingo na kitu kinachoaminika kuwa ni panga na
kisha kuchukua mwili wake na kuuweka kwenye gari la marehemu aina ya
Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY.
“Baada ya
kuuweka mwili wa marehemu kwenye buti alilisafisha gari hilo kwa nje na
kisha kuliendesha mpaka eneo la kikwakwaru “B” kata ya Lemara ambapo
alilitelekeza hapo na kisha yeye kuondoka”. Alifafanua Kamanda Sabas.
“Mara
baada ya gari hilo kukaa mpaka saa 2:00 usiku ndipo baadhi ya wananchi
wa eneo hilo walitoa taarifa kwetu ambapo askari wa doria walikwenda na
kulichukua gari hilo kwa kulivuta mpaka kituoni. Kwa kuwa mke wa
marehemu aitwaye Caroline Lukumay (38) alikuwa anamtafuta mume wake kwa
njia ya simu bila mafanikio ndipo alipoamua kuja kituoni kutoa taarifa
ambapo tulimuonyesha gari lililotelekezwa ambalo alillitambua mara
moja”. Alisema Kamanda Sabas.
Aliongeza kwa kusema kwamba askari
walimuomba mke wa marehemu funguo za akiba za gari hilo ambapo baada ya
kulifungua ndipo walipouona mwili wa marehemu kwenye buti akiwa na vitu
mbalimbali kama vile simu mbili aina ya Sony na Panasonic, pesa taslimu
Tsh 300,000, Laptop aina ya Asus na kadi za benki tofauti tofauti.
Mara
baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa alikiri kuhusika na mauaji hayo na
kusema siku hiyo walikuwa wawili tu yaani yeye na mrehemu na alifanya
hivyo kwa kuwa alikuwa na tamaa za fedha alizokuwa nazo marehemu ndani
ya nyumba hiyo kiasi cha Tsh. Mil.5.
Upekuzi zaidi wa Jeshi la Polisi
ulibaini kuwepo kwa fedha taslimu Tsh. 4,294,000, simu tatu aina ya
Sumsang na vocha za mtandao wa vodacom za sh. Elfu tano tano zenye
thamani ya Tsh. 70,000 ambapo vyote vilifukiwa kwenye banda la kuku.
Mbali
na vitu hivyo pia mtuhumiwa Ismail Swalehe Sang’wa aliweza kuonyesha
panga lenye damu ambalo alilihifadhi stoo pamoja na taulo nne kubwa,
kitambaa cha mezani na suruali yake ambazo zilikuwa na damu na
alizitumia yeye mwenyewe kupigia deki sebuleni baada ya tukio na kisha
kuzificha kwenye migomba karibu na mabanda ya kuku.
Kamanda
Sabas alimalizia kwa kusema kwamba Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa
watatu wengine mbali na Ismail Swalehe Sang’wa akiwemo mke wa marehemu,
rafiki wa mke wa marehemu ambaye ni mwanamke na dereva wa nyumbani wa
marehemu kwa mahojiano zaidi.
0 comments:
Post a Comment