Ni furaha ya kila mzazi kupata mtoto mwenye siha njema na mtimilifu wa viungo. Lakini ilikuwa bahati mbaya kwa Mario Sanga, ambaye licha ya kubarikiwa kupata mtoto wa kiume mwenye afya bora, aliyekamilika, kufumba na kufumbua mtoto huyo amepata ulemavu ambao ni adhabu pia upungufu mkubwa kwa mwanaume yeyote duniani.
Ulemavu huo si kama ule
wa kukosa mikono, miguu, macho au ulemavu wa ngozi bali ni kitendo
cha mtoto huyo kukosa uume baada ya kukatwa na daktari wakati wa tohara.
Jambo hilo pengine litamkosesha mtoto huyo kuwa baba na kufurahia maisha ya ndoa kama wanaume wengine.
Ilivyotokea
Sanga,
mkazi wa Mang’ula, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro anaeleza kuwa
siku ya tarehe 15 ya Juni mwaka 2012, alimpeleka mtoto wake (jina
linahifadhiwa) hospitali kwa ajili ya kufanyiwa tohara.
Alipofika
hapo kama ilivyo ada, alipokelewa na madaktari ambao walimchukua mtoto
na kumwingiza katika chumba maalum kwa ajili ya tohara. “Ilituchukua
nusu saa tu, baada ya kuingia ndani na mtoto na kuanza kumfanyia tohara,
baadaye daktari alitoka na mtoto, lakini alikuwa akitokwa damu kwa
wingi. Kwangu mimi lile jambo halikuwa la kawaida,” anasema Sanga.
Anasema
kuwa daktari wa hospitali hiyo, aliyemtaja kwa jina la Castory Magoha,
hakuwaeleza chochote zaidi ya kuwaambia kwamba mtoto wao ametokwa damu
nyingi na kuwaagiza kuwa endapo damu itaendelea kutoka wamrudishe
hospitali hapo.
Kwa maelezo ya Sanga, damu iliendelea
kumtoka mtoto wao kwa wingi na walimrudisha hospitali na daktari
aliwapa rufaa ya kwenda kwenye hospitali ya daktari mwingine aliyetajwa
kwa jina la Mgonyi ambaye kwa sasa ni marehemu.
Sanga
akiwa na mtoto wake walikwenda hadi kwa daktari waliyeelekezwa na
walipofika, Dk Mgonyi alimchunguza mtoto, bila kumpa tiba yoyote na
kuwaambia warudi kwa daktari aliyemfanyia tohara. “Tuliporudi kwenye
hospitali ya kwanza, Dk Magoha alituandikia sindano na kutuambia turudi
tena baada ya wiki mbili, wakati huo mtoto likuwa akilia sana kwa
maumivu,” anasema.
Anabainisha kuwa sindano zilisaidia
kukausha damu, ingawa umbile la mtoto lilionekana haliko sawa ambapo
aliamua kumrudisha kwa Dk Mgonyi kwa uchunguzi zaidi.
“Dokta
(Mgonyi) safari hii hakutuficha, alituambia kuwa mtoto wetu amekatwa
uume, yaani kichwa chote kimeondolewa na alitueleza wazi kuwa, ukataji
wa Dk Magoha ulikuwa na matatizo, ameukata uume wa mtoto badala ya
kufanya tohara ya kawaida,” anasema.
Baada ya kugundua
hilo, Sanga aliamua kufungua kesi katika Kituo cha Polisi cha Ifakara
na baada ya kesi kunguruma kwa miaka mitatu, lakini hukumu ilionyesha
kuwa Dk Magoha hana kosa. Hata hivyo, Sanga hakukubali, aliamua kufungua
kesi nyingine ya madai ya fidia kutokana na daktari huyo kuonyesha
dalili za kukiri kosa. Kabla ya hapo, Sanga anaeleza kuwa Dk Magoha
alimfuata nyumbani kwake na kutaka walimalize tatizo hilo kwa kumlipa
fidia ya Sh5 milioni.
“Wakati kesi ikiwa mahakamani, Dk
Magoha alikuja nyumbani, akaniambia tusameheane na anipe Sh5 milioni.
Mimi nilimkatalia na tukaendelea na kesi, nikashangaa eti ameshinda,”
anasema.
Dk Magoha amshangaa Sanga
Mwananchi
lilipozungumza na Dk Magoha anayedaiwa kumfanyia tohara vibaya mtoto
huyo, alidai kwamba mtoto wa Sanga alizaliwa akiwa na upungufu katika
kiungo hicho, ambao kwa kitaalamu unajulikana kama ‘congenital physical
malformation’.
Dk Magoha alisema hata mahakama
ilishatoa uamuzi na jopo la madaktari liliketi na kukubali kuwa tatizo
la mtoto wa Sanga ni la kuzaliwa nalo.
“Namshangaa,
(Sanga), anaendelea na suala hilo, pengine anataka kunichafua kwa sababu
ninachojua ni kwamba mahakama imeshatoa maamuzi kuhusu hili,” anasema
na kuongeza kuwa, Sanga mwenyewe anafahamu kuwa mtoto wake ana tatizo
hilo na wakati walipompeleka tohara alikiri kuwa hana maumbile ya
kawaida.
Hata hivyo, Sanga anasema endapo mtoto wake
angekuwa na tatizo la kimaumbile, angefahamu mapema kwani alizaliwa
kwenye hospitali kubwa ya Mtakatifu Francis ya Ifakara mkoani Morogoro.
Anaweza kupona?
Pengine
tatizo la mtoto wa Sanga linaweza kupata suluhisho kwani, wataalamu wa
Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini, walifanikiwa
kupandikiza uume kwa kijana wa miaka 21, aliyekatwa uume baada ya
kufanyiwa tohara vibaya, akiwa na umri wa miaka 18. Kijana huyo,
alifanyiwa vibaya upasuaji huo na kusababisha sehemu ya uume huo kuoza.
Kiongozi
wa upasuaji huo, Profesa Andre van der Merwe, alisema upasuaji huo
uliodumu kwa saa tisa, ulifanyika katika Hospitali ya Tygerberg, Cape
Town.
0 comments:
Post a Comment