Mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha juzi usiku imesababisha maafa katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako zaidi ya watu 42 wameuawa, wakiwamo saba wa familia moja na wengine 91 kujeruhiwa vibaya.
Mvua hiyo ya aina yake ilisababisha nyumba 160
kuanguka na nyingine kuezuliwa paa kutokana na upepo mkali na watu
wengine 900 wameripotiwa kukosa makazi.
Watu wengi walifariki kutokana na kuangukiwa na
kuta za udongo za nyumba za wanakijiji hao na wengine kuuawa kutokana na
kuangukiwa na mawe makubwa ya barafu wakati walipokuwa wakijaribu
kutafuta hifadhi baada ya mapaa kutobolewa.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hili
kuwa mawe makubwa ya barafu yalikuwa yakidondoka usiku na kuvunja nyumba
za wakazi wa kijiji hicho ambazo nyingi ni za udongo.
Waokoaji walilazimika kufumua mabati yaliyoanguka
na kufukua vifusi kwa ajili ya kutoa miili ya watu waliofariki na kuokoa
walionusurika na baadaye kuwapakia kwenye malori ili kuwapeleka
hospitalini.
“Mimi tangu nianze uongozi wa umma sijawahi kukutana na tukio la aina hii,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya.
“Nashindwa kulizungumzia (suala hili). Hili ni
tukio kubwa ambalo limepoteza uhai wa maisha ya watu hivyo nashindwa
nianzie wapi lakini kifupi wananchi wa Mwakata wamekumbwa na msiba
mzito,” alisema Mpesya, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya
Wilaya.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ezekiel Sanane alisema
wakati mvua hiyo inanyesha ilikuwa na upepo mkali na mawe makubwa
ambayo yalikuwa yakitoboa nyumba na kutumbukia ndani na kuponda watu,
hali ambayo iliwafanya wengine kukimbilia nje ambako pia walipigwa na
mawe ya barafu na kufariki.
Sanane alisema wapo wengine walifunikwa kabisa na ukuta wa nyumba na kufariki, lakini wengine wamekufa wakiwa nje ya nyumba zao.
Hata hivyo mkazi wa kijiji hicho, Paulina Nyalulu
alisema alinusurika kifo baada ya kukimbilia barabarani. Alisema baada
ya kuona nyumba imejaa maji, yeye na familia yake walikimbilia
barabarani ambako walishuhudia nyumba zao zikianguka, ingawa hakuna mtu
aliyekufa.
“Tunamshukuru Mungu hakuna aliyekufa kwenye
familia hii lakini kama unavyoona vitu vyote, vikiwemo vyombo pamoja na
vyakula vimezolewa vyote maana maji yalijaa nyumba yote na sisi
tulikimbia na ndiyo ilikuwa usalama wetu,” alisema Nyalulu.
Taarifa za awali zilizotolewa na kamanda wa polisi
wa Mkoa wa Shinyanga, Jastus Kamugisha zilieleza kuwa idadi hiyo
inaweza kuongezeka kutokana na kazi ya kufukua miili kutoka kwenye
vifusi vya nyumba kuendelea hadi jana mchana.
0 comments:
Post a Comment