Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati patamu’ ulioimbwa na Msanii Ney wa
Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili.
Msanii huyu amekuwa na tabia na mienendo
yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya
maonesho yenye kukiuka maadili. Kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu
wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada
mbalimbali.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu
namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu
la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au
wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.
ikumbukwe kwamba BASATA limeshamuita na
kumuonya msanii huyu mara kadhaa kutokana na tabia yake ya kutoa kazi
zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo. Kwa
hiyo kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba
hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa
kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. Kwa
sasa Msanii huyu ametoa wimbo mwingine wa Pale Kati patamu ambao uko mitandaoni
ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa
mnyama.
Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia
wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa na wasanii genge la
wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa jamii. BASATA linapenda kueleza
ya kufuatayo
• BASATA linatamka kuwa limeufungia wimbo
huu rasmi kutumika kwa namna yoyote ile.
• Aidha pamoja na adhabu ya kufungia
wimbo huu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote
nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao.
SANAA NI KAZI, TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI.
0 comments:
Post a Comment