SHANGWE!
Katika tukio linalotokea kwa nadra, wazee kumi ambao wameishi kinyumba
kwa miaka mingi,Jumamosi iliyopita walibariki ndoa zao katika Kanisa
Katoliki Parokia ya Mtakatifu Monica, lililopo Tungi mkoani Morogoro,
huku zoezi hilo likitikisa kila kona ya mjini hapa.
Kwa mujibu wa padri aliyefungisha ndoa
hizo, Ferdinand Mushi, tukio hilo lilifanyika baada ya ushawishi wa muda
mrefu wa viongozi wa Kigango cha Mt. Clara kwa wazee hao, ambao awali
walifanya doria ya nyumba hadi nyumba ili kubaini watu wanaoishi bila
ndoa za Kikristo.
“Naomba Vigango vingine hapa Morogoro na
Tanzania kwa ujumla kuiga mfano wa Mt. Clara, ambao waliamua kuwapa
semina na kukubali kufunga ndoa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigango
hicho, Gilbert Robert alisema wao kama viongozi, wajibu wao ni
kuwaelekeza waumini kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, kwani kabla ya
kufanikisha zoezi hilo, walifanya sensa na kugundua uwepo wa familia 44
zinazoishi bila ndoa, lakini ni kumi tu kati yao ndiyo walikubali
kubariki.
“Baadhi waligoma wakidai hawana fedha za
kufanya sherehe, hivyo sisi Kigango tumeamua kuwafanyia sherehe kwenye
ukumbi huu wa masista,” alisema mwenyekiti huyo.
Wakati wa sherehe hizo ukumbini,
wanandoa hao, wapambe, ndugu na jamaa waliburudika kwa chakula aina ya
pilau na soda, huku kukiwa na vituko vya hapa na pale ikiwa ni pamoja na
mabusu ya kizee kutawala.
Baada ya sherehe hiyo, wakati wa kurejea
makwao tulishuhudia baadhi yao wakitembea kwa miguu huku akina mama
wakizikunja shera zao, ingawa pia baadhi yao waliondoka kwa bodaboda,
tena wakiwa wamepakizana kwa staili maarufu ya mishikaki.
0 comments:
Post a Comment