MPENZI msomaji wa Love & Life napenda kukukaribisha katika mada nzuri ya wiki hii inayosema siku moja, kila mpenzi ashinde na simu ya mwenzake…tuone!
Nianze kwa kusema tu, naamini mada hii itakuwa ni ngumu sana kwa wapenzi wa zama hizi za kizazi kipya, bila kujali wahusika kama ni wapenzi, wachumba au wanandoa, bado ugumu nauona akilini mwao.
Kwa nini?
Kama kweli mnapendana hakuna ugumu wowote, ila ugumu unakujaje? Ninaamini kama utamuachia mpenzi wako simu yako, kwa tabia zako za kutokuwa mwaminifu, ni hakika atakutana na madudu mengi sana na hapo ndipo ugumu wa kumwachia mwenza wako simu yako unapoanzia.
Simu ni chanzo kweli?
Kama ulikuwa hujui tambua sasa kwamba, katika ulimwengu huu wa utandawazi, simu imekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kusababisha kuvunjika kwa ‘mahusiano’ miongoni mwa wapendanao.
Hii yote inachangiwa na kuwepo kwa mitandao mbalimbali ya kijamii kwa nia ya kurahisisha mawasiliano.
Tatizo kwenye mitandao kila mtu mzuri
Kwa mitandao mingi, iwe WhatssAp, Twitter, Facebook, Badoo, Instagram na mingine mingi, kila mtu anajitahidi kuweka picha nzuri itakayomuonesha yeye akiwa mrembo (kama ni mwanamke) au mtanashati (kama ni mwanaume). Hii yote ni kwa ajili ya kuwavutia michepuko.
Sasa utakuta mtu tayari yupo kwenye uhusiano lakini akavutiwa na mwingine wa kwenye Facebook, basi wanaunga hapohapo na usaliti unaanza.
Kila mtu na simu yake
Ni jambo la kawaida kwa wapenzi, wachumba au wanandoa kila mtu kuwa bize na simu yake kwa muda wote na kila mtu hayuko tayari kuona mwenzake kashika simu yake. Ndiyo maana walio wengi unakuta wameweka namba za siri (password) ili hata kama mwenza wake ataishika basi asiweze kuzama ndani na kutazama chochote bila idhini yake, hasa michepuko ya kwenye mitandao.
Miujiza itokee
Natamani siku moja, kila mmoja katika wawili walio kwenye uhusiano ashinde na simu ya mwenzake. Watakaofanikiwa na siku ikapita salama bila kukumbana na vimeo au michepuko ya aina yoyote ile, naamini uhusiano wao utachipuka upya na kuaminiana na penzi lao litadumu.
Angalizo
Kama hizi simu tusipoziangalia na kuzitumia vizuri kwa ajili ya kudumisha uaminifu na kujenga uhusiano ulio bora, basi kizazi hiki kitavunja rekodi kwa wawawili walio kwenye uhusiano wa kimapenzi kutokuwa waaminifu na au uhusiano wao kuvunjika.
SOURCE:GPL
0 comments:
Post a Comment