Shahidi wa nne katika kesi ya tuhuma za ubakaji inayomkabili Emmanuel Mbasha, mume wa mwanamuziki wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, jana alidai mahakamani kuwa hakuona dalili zozote za kuingiliwa kimwili mlalamikaji.
Hayo yalidaiwa na daktari wa Hospitali ya Amana, Migole Mtuka, ambaye alimfanyia vipimo msichana huyo.
Daktari huyo
alidai katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwamba vipimo alivyomfanyia
msichana huyo anayedaiwa kubakwa na Mbasha, havikuonyesha kitu chochote.
Dk. Migole alidai kuwa binti huyo alifika hospitalini hapo Mei 26, mwaka jana, kwa alili ya kufanyiwa vipimo.
Alidai kwamba
binti huyo alipofika hospitalini hapo, alimfanyia kwanza vipimo vya
macho kisha kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, ambavyo hutolewa
bure.
Dk. Migole
alidai kwamba baada ya kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, akiwa
na baadhi ya ndugu wa familia yake, hakwenda bali aliingia mitini na
kurejea Juni 3, mwaka jana, baada siku nane kupita.
Alidai baada ya
kufanyiwa hivyo, vipimo hivyo vilionyesha kuwa hakuna kitu chochote
alichofanyiwa, kwa maana ya kubakwa au kuingiliwa na mwanamume katika
mwili wake na kuwajazia fomu aina ya PF3 kwa kile alichokiona.
“Binti huyo
hakuonekana kuwa na ujauzito, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na
wala mbegu za kiume katika sehemu za siri,” alidai daktari huyo.
Hata hivyo,
baada ya kutolewa ushahidi huo, Hakimu Flora Mujaya, hawakuweza
kusikiliza ushahidi mwingine kutokana na taarifa za msiba wa hakimu
mwenzao, zilizofika mahakamani hapo.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa upande wa Jamhuri Aprili 20, mwaka huu.
Mbasha anadaiwa
kuwa Mei 23 na 25, mwaka jana, alimbaka binti mwenye umri wa miaka 17,
ambaye anadaiwa ni shemeji yake huku akijua kufanya hivyo ni kinyume
cha sheria.
0 comments:
Post a Comment