Muziki,Habari motomoto,MICHEZO,Maajabu,Picha Picha na mambo mengine mengi hapa ndani ya KALI ZA DJ YEYO

nongona

tangazo eligod

tangazo eligod

About the Author

CHECK me!!!!

CHECK me!!!!

Sunday, December 28, 2014

Utajuaje kama mwanamke uliyenaye anakupenda?


.
MARAFIKI zangu karibuni tena katika ukurasa wetu wa huba, ambao kwa hakika umekuwa tiba ya matatizo yaliyopo katika uhusiano wako. Sina shaka kwamba, mbali na kukupa tiba ya matatizo yako, lakini pia ni darasa maridhawa katika kuboresha na kutambua jinsi sanaa ya mapenzi ilivyo.

Sijisikii woga kusema kwamba ukiwa mdau wa ukurasa huu, utakuwa mjanja wa mapenzi na kamwe hutasumbuka kutafuta penzi la kweli. Nikunong’oneze kwamba, kitabu changu cha Joseph Shaluwa...Let’s Talk About Love kinaendelea kupikwa, endelea kuvuta subira, kitakufikia hivi karibuni.

Humo utajifunza kikamilifu mambo mbalimbali juu ya mapenzi, uhusiano na ndoa. Utapata dawa ya mpenzi msaliti na namna ya kumfanya mpenzi wako awe wako peke yako. Zaidi ya yote, utapata Love Messages nyingi ambazo zitazidi kupalilia penzi lako na mwandani wako na kulifanya kuwa bora kila siku.

Naam! Sasa tunarejea katika mada yetu ya leo...ninaongea na wanaume ambao wanapenda kufahamu kama wenzi wao wanawapenda kwa dhati. Rafiki zangu mnajua mapenzi ni kama mchezo wa kujificha na kutafutana? Yaani hauna kanuni maalum, unaweza kukimbilia huku lakini mwenzako akahangaika sehemu nyingine akikusaka!

Ingekuwa hisia ni rahisi kama sauti, basi mtu angesimama juu ya mlima mrefu na kupiga kelele lakini si hivyo. Ni mchezo unaohitaji mbinu nyingi, umakini wa hali ya juu na utulivu uwanjani! Hautaki papara.

Wengi leo hii wapo kwenye uhusiano ambao hawana uhakika nao, utakuta mtu yupo na mwanamke ambaye hajui kama anampenda kama anavyompenda yeye au lah! Hilo ni tatizo, maana unaweza kuendelea kupoteza muda wako kwa siku nyingi, lakini mwisho akakutosa na kukuacha vibaya ukiwa bado hujajiandaa kuachwa!

Ipo mifano mingi, nimeongea na wengi kwenye simu na hata ana kwa ana, kilio chao ni hicho hicho, wametendwa na wenzi wao ambao wamekuwa nao kwa muda mrefu sana wakiamini kwamba wanawapenda kumbe ni kinyume chake.

Mbaya zaidi ni kwamba wakati wakiachwa wanakuwa tayari wameshawagharamia vitu vingi vya thamani, fedha n.k, hapo unakuwa mwanzo wa kuchanganyikiwa na kuharibu kila kitu katika maisha yao! Naam...sasa nakupa mbinu muhimu zaidi zilizopendekezwa na wataamu wa Saikolojia ya Mapenzi, zitakazoweza kukusaidia kutambua kama mwanamke uliyenaye ana mapezi ya kweli kwako.

Zipo ishara ambazo mwanamke akizifanya utaweza kufahamu ameegemea upande gani katika penzi lenu! Hapa chini ni baadhi ya ishara unazotakiwa kuziangalia unapokuwa na mwanamke katika mahusiano (hasa nyakati za mwanzoni) kabla hujaamua kuingia kichwa kichwa. Hebu tuzione.

KUJITOA KWA KILA HALI
Kama mwanamke anakupenda kwa dhati, atajitoa kwako kwa kila hali. Unajua, kuna mambo ambayo si rahisi kufanyiwa na kila mtu, yapo ambayo yanafanywa kwa watu wanaopendana tu. Huyu atajitoa kwako.

Atafanya mambo muhimu ambayo si rahisi kuyafanya kwa mtu mwingine. Anatakiwa kukupa vipaumbele kwenye mambo yake yote. Kwa kukueleza mipango yake (hata ile ya siri) na kukufanya wa kwanza kujua kinachoendelea katika maisha yake.

Lazima ujiulize na uangalie, je, wewe ni moja ya vipaumbele vyake? Je, wewe unakuwa wa kwanza kujua mambo yake kabla ya rafiki zake? Je, uzito anaochukulia kwako ukiwa na tatizo, ndiyo anaouchukua pia kwa rafiki zake ama ndugu zake? Lazima kuwe na tofauti. Siku zote, umuhimu wako hauwezi kuwa sawa na mfanyakazi mwenzake ofisini.

Mwanamke wa aina hii, ni rahisi kukuambia: “Nachukia jinsi kaka yangu anavyompiga mdogo wetu wa mwisho. Ni tabia mbaya inayonikosesha usingizi.” Unaweza kuona ni jambo dogo, lakini fahamu kwamba amekufanya rafiki na kukueleza mambo ya ndani kabisa ya familia yake. Anafanya hivyo kwasababu anakuamini, anajua wewe ni yeye na yeye ni wewe! Upo rafiki yangu? Hebu tuone kipengele kingine hapa chini...

WASIWASI NA USALAMA WAKO
Baadhi ya wanawake wanaweza kusema mengi lakini wasiwasi kwa ajili ya usalama wa mtu unayempenda ni muhimu sana. Hii ni moja ya njia ya kujua kama mwanamke anakupenda. Anapenda kujua uko wapi, unafanya nini na utarudi nyumbani muda gani?

Si rahisi kufanya hivyo kwa mwanaume ambaye hana mapenzi naye. Anafanya kwako, kwasababu anakupenda na anajali usalama wa maisha yako, na si maisha yako pekee, bali kuna jambo kubwa na zito zaidi; ANAJALI USALAMA WA PENZI LAKE maana hataki kukupoteza na kulipoteza penzi hilo!

WIVU
Ingawa si lazima awe na wivu lakini inaelezwa kwamba wivu ni moja ya alama ambazo unatakiwa kuziangalia wakati ukimchunguza kama anakupenda kwa dhati. Wivu ni ladha ya mapenzi. Ni kama ndimu kwenye mchuzi au kitunguu swaumu kwenye pilau! Unaonaeeeh?!
Wivu ni afya ya uhusiano, kwamba lazima aoneshe wasiwasi na wewe, atilie mashaka simu yako, achunguze email yako, blog na hata ukurasa wako wa Facebook! Hana nia mbaya, lakini anachotaka kujua, ni kweli yupo peke yake?

Zipo ishara nyingi, sana nyingine za kawaida ambazo wewe mwenyewe unaweza kuzijua bila kufundishwa, ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaonesha kwamba anakuonea wivu. Alama hii ni muhimu sana kwa mpenzi ambaye anakupenda kwa dhati. Zipo nyingine nyingi, lakini kwa leo tunaishia hapa, wiki ijayo tunaendelea na ishara nyingine.

Kama una kesi nyingine za mambo ya mahusiano ya mapenzi, unataka kujua kama mwanamke wako ana upendo wa kweli kwako, anakusaliti, kujua mambo ambayo ukiyafanya utamvutia mwenzi wako katika uhusiano.

Kugundua nguvu, hatua kwa hatua ya siri ya jinsi ya kukutana, kuvutia, na kujenga uhusiano bora wa kudumu na kutimiza lengo lako la kuingia kwenye ndoa, endelea kuwa mdau mkubwa wa ukurasa huu, pia tafuta vitabu vyangu kwa mada nyingi zaidi. Hadi wiki ijayo tena katika sehemu ya pili, hapa naweka nukta.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;

0 comments: