TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tunazo taarifa kuwa Rais Kikwete amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio
cha uchunguzi wa Ikulu, ili kuwalinda watuhumiwa ambao wanapaswa
kuwajibishwa kwa kuwafuta kazi, kushitakiwa na kufilisiwa. Habari
tulizozipata kutoka ndani ya Ikulu kwenyewe, zinasema Rais Kikwete
amejiandaa kumlinda Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Tunapenda kumtahadharisha Rais Kikwete kuachana mara moja na mpango
wowote wa kumlinda Profesa Muhongo na Maswi, ambao hadi muda huu
walipaswa siyo kuwa nje ya ofisi, bali walitakiwa kuwako gerezani.
Ndugu waandishi wa habari; Umma unafahamu kwamba anayejiita mmiliki wa
Kampuni ya PAP, alikabidhiwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow,
kabla ya kuwa mmiliki halali wa kampuni hiyo.
Ushahidi wa hili, unapatikana katika kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya
Tanzania na James Rugemalira, dhidi ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof.
Benno Ndulu, Kampuni ya PAP na Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.
Rugemalira alifungua shauri hili baada ya kukuta fedha zilizokuwapo
kwenye akaunti ya Escrow zimeshachukuliwa, wakati yeye akiwa bado
hajamaliziwa kiasi chake cha fedha alichokuwa anadai baada ya kuuza
asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL.
Katika shauri hilo lililomalizika kwa njia ya usuluhishi wa mahakama,
Mahakama Kuu ya Tanzania, pamoja na mengine, ilisema yafuatayo:
·Kwamba baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake zilizotajwa katika
mkataba, itailipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi yote ya
mapato inayotokana na mkataba inayofikia Sh. 38, 186,584,322/- (bilioni
thelathini na nane milioni mia moja na themani na sita laki tano na elfu
themanini na nne na mia tatu ishirini na mbili) kama zilivyokadiriwa na
TRA kupitia Kadirio la Kodi Na. 427038820 la tarehe 15 Januari 2014.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani tarehe 8 Januari 2014 na VIP
ENGINEERING AND MARKETING LIMITED (VIP) kama mdai na iliunganisha kesi
za madai Na. 49/ 2002 na kesi ndogo Na. 254 YA 2003.
· Kwamba baada ya VIP kulipa kodi hiyo kwa TRA, fedha zake zilizobaki
hazitalipwa kwake mpaka pale itakapowasilisha Cheti cha Kulipa Kodi na
hati za kuhamisha asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL kwa mwanasheria
wa PAP, na wasilisho hilo lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10 jioni ya
tarehe 27 Januari 2014.
·Aidha, baada ya kulipwa kiwango chote cha mkataba kilichotajwa hapo
juu, VIP itathibitisha uridhiaji na ukubali wake wa kuhamishwa asilimia
70 ya hisa za MECHMAR CORPORATION (MALAYSIA) BERHAD katika IPTL, na
uridhiaji na ukubali huo unarudishwa nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na
uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.
Ndugu waandishi wa habari; Hii maana yake nini? Jibu ni kwamba,
wakati PAP analipwa kiasi cha Sh. 321 bilioni kutoka BoT, haikuwa
mmiliki halali wa IPTL. Hakuwahi kusajili hisa zake BRELA wala hakuwa
amenunua asimia 30 ya hisa za VIP.
Huu ni wizi ambao hauwezi kuvumiliwa na umma na chama chetu, ambacho ni
tegemeo la Watanzania katika kulinda rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha
na kutetea haki za wanyonge na kusimamia misingi ya uwajibikaji,
hakiwezi kunyamaza na kumuacha Rais Kikwete akitekeleza mradi wake wa
kulinda wezi.
Hakiwezi! Kwa msingi huo, tunamtaka Rais Kikwete katika hotuba yake ya
kesho, kuwajibisha wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine,
katika kutekeleza wizi huo. Miongoni mwao, ni Prof. Muhongo, Maswi,
Gavana wa BoT, Prof. Ndulu, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Silviacius
Likwelile, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Fredric Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba.
Ndugu waandishi wa habari, Watanzania bado wanakumbuka kauli
iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita kuwa familia ya Rais
Kikwete nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa mnufaikaji mkubwa kupitia
kwa mtu aitwaye Albert Marwa ambaye ana uhusiano na familia hiyo.
Kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua madhubuti katika jambo
hili, utakuwa ni ushahidi wa wazi kuwa kigugumizi ambacho kimekuwa
kikiikabili serikali yake katika jambo hili kinasukumwa na jambo kubwa
nyuma yake, ikiwamo kujilinda binafsi na kulinda familia yake.
Ndugu waandishi wa habari, Suala la miamala iliyofanyika kupitia Benki
ya Stanbic katika sehemu ya kashfa hiyo ya Akaunti ya Escrow, si suala
la kufanyia mzaha au kupuuzwa hata kidogo katika ufisadi huu.
Ni kupitia benki hiyo ndiko kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160
bilioni, zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku
moja mchana kweupe, tena tunaambiwa wengine walikwenda kwa magari yenye
nambari za serikali na fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako Rais Kikwete
anafanyia kazi na kuishi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna benki ndani ya nchi yetu inayoweza
kufanya miamala ya mabilioni ya fedha kwa kiwango hicho, bila BoT
kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo hiyo, Gavana Prof. Ndulu hawezi kukwepa
uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na kulilidhia.
Tunatarajia Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania hatua
zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa wa umma na siyo kuja na
visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi pekee.
Watanzania wanasubiri kusikia Rais Kikwete anachukua hatua dhidi ya
Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum ambaye wakati fedha zinaztolewa katika
Akaunti ya Escrow kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, alikuwa ndiye
Kaimu Waziri wa Fedha.
Wakati huo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alikuwa Afrika
Kusini kwenye matibabu ya ugonjwa uliopelekea kifo chake ambacho hadi
leo kimeendelea kudaiwa kuwa na utata.
Ndugu waandishi wa habari; Aidha, katika kuwatafuta watu waliochukua
fedha za Akaunti ya Escrow kwa magunia na malumbesa, Rais Kikwete aweke
wazi kile kinachoonekana ushirika wa ufisadi kati ya serikali, Benki ya
Stanbic na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu Mkuu
wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Tunazo taarifa za uhakika kwamba Kinana alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Benki hiyo na Mjumbe wa Bodi ya Stanbic, na ambaye amekuwa kiunganishi
kikubwa kati ya serikali, CCM na benki hiyo katika kufanya miamala ya
aina hiyo ya kifisadi.
Umma wa Watanzania unamtarajia Rais Kikwete amwagize Kinana, kwa
ushawishi wake alionao ndani ya Stanbic, awataje watu waliokwenda
kuchukua mabilioni ya fedha kwa malumbesa, magunia na sandarusi,
vinginevyo atakuwa anahalalisha madai haya kuwa ushirikiano huu una kitu
nyuma na kwamba, fedha kutoka Akaunti ya Escrow ya Tegeta, kupitishiwa
benki hiyo halikuwa jambo la bahati mbaya.
………………………
Arcado Ntagazwa
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI CHADEMA
0 comments:
Post a Comment